Baada ya masikitiko katika dakika za mwisho dhidi ya Bayern Munich wakati
wa mechi yao ya kwanza Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya ngazi ya makundi,
Manchester City hawawezi hawatakuwa tayari kuteleza tena watakapokutana na
Roma kesho Jumanne uwanjani Etihad.
Bao la dakika ya 90 la kijana wa zamani wa City Jerome Boateng
liliwatunuku Bayern ushindi wiki mbili zilizopita, na baada ya Roma
kuanza kampeni yao Kundi E kwa kuiponda CSKA Moscow 5-1, mabingwa hao wa
Uingereza tayari wanakabiliwa na presha kiasi.
Baada ya kurarua Sheffield Wednesday 7-0 katika League Cup kabla ya
kulaza Hull City 4-2 ligini Jumamosi, vijana hao wa Manuel Pellegrini
wanafunga mabao mengi, lakini mkabaji wa kulia Pablo Zabaleta anajua
Roma watakuwa tofauti.
“Sasa tunahitaji kufungua ukurasa mwingine na kufikiria tu kuhusu
Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya,” beki huyo wa kulia wa Argentina aliambia
televisheni ya City baada ya ushindi dhidi ya Hull.
“Tulipoteza mechi dhidi ya Bayern Munich na sasa tutakabiliana na Roma nyumbani. Tunajua umuhimu wa kushinda mechi hiyo.
“Itakuwa mechi nyingine ngumu kwa sababu Roma pia ni wazuri, tunatumai tutacheza vyema na kupata alama tatu.”
Kihistoria, Roma hawajakuwa na matokeo mema dhidi ya klabu za
Uingereza.
Walishindwa kupitia mikwaju ya penati na Liverpool mara yao pekee
kucheza fainali ya ubingwa Ulaya 1984 na wameshinda moja peke kati ya 14
walizocheza Uingereza.
Manchester ulikuwa pia mji waliopokezwa mojawapo ya vichapo vikubwa
zaidi walipolazwa 7-1 na wapinzani wa City jijini Manchester United
kwenye robo fainali ya Ligi ya Klabu Bingwa Ulaya 2007.
Lakini ingawa City hawajawahi kulazwa na klabu ya italia katika mechi
nne za majuzi, zaidi watatahadhari sana dhidi ya timu hiyo ambayo sasa
inapigania ubabe wa Serie A na Juventus.
Vijana hao wa Rudi Garcia wameshinda mechi zao zote sita walizocheza
katika ligi msimu huu, ikiwa ni pamoja na ushindi wa 2-0 dhidi ya Hellas
Verona uliowaweka sawa kwa alama na Juventus kileleni kabla ya kivumbi
kati ya timu hizo mbili mjini Turin wikendi hii.
Ushindi wa Jumamosi dhidi ya Verona ulifanya Garcia kufikia alama 100
Serie A katika mechi yake ya 43 kileleni – mapema kushinda kocha
mwingine yoyote wa awali Roma – na anasema klabu yake itazuru Manchester
ikiwa bila wasiwasi.
"Itakuwa mechi kubwa. Hawana alama, hivyo ndio walio na presha.
Wanahitaji matokeo kwao nyumbani,” alisema Mfaransa huyo, ambaye vijana
wake walimaliza wa pili nyuma ya Juve nchini Italia msimu uliopita.
"Tuko thabiti na tumeonyesha kuwa na imani kubwa katika uchezaji
wetu.
Tuko tayari kukabili changamoto zinapochipuka, lakini lazima
tufurahie mechi hii na kubeba kile tutakachofanikiwa.”
No comments:
Post a Comment