Release No. 099
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
Juni
26, 2012
TFF KUZAWADIA WAPIGA PICHA
COPA COCA-COLA
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) litawazawadia wapiga picha za magazetini watakaoripoti mashindano
ya Copa Coca-Cola 2012 ngazi ya Taifa yanayoendelea kwenye mikoa ya Dar es
Salaam na Pwani.
Mashindano hayo
yanayodhaminiwa na Kampuni ya Coca-Cola na kushirikisha mikoa 28 yanafanyika
viwanja vya Tanganyika Packers, Kumbukumbu ya Karume mkoani Dar es Salaam, na
viwanja vya Tamco na Nyumbu mkoani.
Zawadi ya sh. 250,000
itatolewa kwa picha bora katika maeneo matatu; action picture, fair play picture
na mpiga picha ambaye ameripoti matukio mengi ya mashindano hayo
yanayoshirikisha vijana wenye umri chini ya miaka 17.
Washiriki wanatakiwa
kuwasilisha picha zao zilizotumika (cuttings) ofisi za Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF).
NGORONGORO HEROES KUJIPIMA
KWA MISRI, RWANDA
Timu ya Taifa ya vijana wenye
umri chini ya miaka 20 (Ngorongoro Heroes) itacheza mechi nne za kirafiki na
timu za Misri na Rwanda kabla ya kuivaa Nigeria kwenye mashindano ya
Afrika.
Ngorongoro Heroes ambayo kwa
mara ya kwanza itakuwa chini ya kocha mpya Jakob Michelsen itaanza kwa kucheza
mechi mbili za Misri zitakazofanyika Julai 3 na 5 mwaka huu, na baadaye Julai 14
na 16 mwaka huu dhidi ya Rwanda.
Mechi zote zitachezwa nchini,
na kama ilivyo Ngorongoro Heroes, Misri na Rwanda nazo ziko kwenye
kinyang’anyiro cha kusaka tiketi za kucheza Fainali za Afrika kwa vijana wenye
umri chini ya miaka 20 zitakazofanyika mwakani nchini Algeria.
Katika raundi ya kwanza,
Ngorongoro Heroes iliitoa Sudan ambapo katika raundi ya pili imepangiwa Nigeria,
na mechi ya kwanza itafanyika jijini Dar es Salaam, Julai 29 mwaka huu. Timu
hizo zitarudiana wiki mbili baadaye nchini Nigeria.
Iwapo Ngorongoro Heroes
itafanikiwa kuitoa Nigeria, katika raundi ya mwisho itacheza na mshindi kati ya
Congo Brazzaville na Afrika Kusini.
MABINGWA COPA WALALA KWA
RUVUMA
Ruvuma imeanza vizuri
michuano ya Copa Coca-Cola baada ya kuwafunga mabingwa watetezi Kigoma mabao 2-0
katika mchezo wa kundi A uliofanyika leo asubuhi (Juni 26 mwaka huu) kwenye
Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam.
Kigoma ambayo iliifunga Lindi
mabao 2-0 katika mechi ya ufunguzi iliyochezwa juzi, ilishindwa kufua dafu mbele
ya Ruvuma na kuruhusu bao katika kila kipindi.
Mabao yote ya washindi
yalifungwa na mshambuliaji Edward Songo. Mshambuliaji huyo alifunga bao la
kwanza dakika ya 34 wakati la pili alilipachika dakika ya 84.
Katika mechi nyingine
zilizochezwa leo asubuhi, Tanga na Morogoro zilitoka sare ya mabao 3-3 katika
mchezo uliofanyika Uwanja wa Tanganyika Packers ulioko Kawe, Dar es
Salaam.
Mkoani Pwani, Mara iliifunga Temeke bao 1-0
kwenye Uwanja wa Nyumbu wakati Kagera ililala bao 1-0 mbele ya Kilimanjaro
katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Tamco.
TFF YAMTAMBULISHA KOCHA MPYA
WA VIJANA
Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) limemtambulisha rasmi leo mbele ya waandishi wa habari kocha mpya
wa timu za Taifa za vijana, Jakob Michelsen kutoka Denmark ambaye amechukua
nafasi ya Kim Poulsen ambaye hivi sasa anainoa Taifa Stars.
Michelsen ambaye amepewa
mkataba wa mwaka mmoja alitambulishwa na Katibu Mkuu wa TFF, Angetile Osiah na
kusema falsafa yake ni kama ile ya Poulsen ya kumiliki mpira na kushambulia muda
wote wa mchezo.
Kabla ya kuja Tanzania,
Michelsen alikuwa kocha wa timu ya daraja la kwanza ya Hobro IK ya Denmark. Ana
leseni A ya ukocha kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Ulaya (UEFA), leseni ya
ukocha wa vijana kutoka Chama cha Mpira wa Miguu cha Denmark (DBU).
Moja ya mafanikio yake ni
kuipa ubingwa wa Denmark, timu ya Skovbakken kwenye ligi ya timu zenye umri
chini ya miaka 18. Ubingwa huo aliupata msimu wa 2005/2006.
Boniface
Wambura
Ofisa
Habari
Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment