Mechi ya Simba na URA
ya Uganda kuwania Klabu bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame)
iliyokuwa ichezwe Jumatatu (Julai 16 mwaka huu) sasa itafanyika Jumapili (Julai
15 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Baraza la Vyama vya
Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) limefanya mabadiliko hayo
kutokana na fainali ya Copa Coca-Cola 2012 iliyokuwa ichezwe kwenye uwanja huo
kuhamishiwa Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Kutokana na
mabadiliko hayo, mbali ya mechi ya Simba na URA itakayoanza saa 10 kamili
jioni, mechi nyingine Jumapili itakuwa kati ya Vita Club ya Jamhuri ya
Kidemokrasi ya Congo (DRC) dhidi ya Ports ya Djibouti itachezwa saa 8 kamili
mchana Uwanja wa Chamazi.
Pia siku hiyo hiyo ya
Jumapili kwenye Uwanja wa Chamazi kutakuwa na mechi nyingine itakayoanza saa 10
kamili jioni. Mechi hiyo itazikutanisha timu za Azam ya Tanzania Bara na
Mafunzo kutoka Zanzibar.
Mechi za ufunguzi wa
mashindano hayo Jumamosi (Julai 14 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam zitabaki kama zilivyopangwa awali. Mechi ya kwanza saa 8 mchana itakuwa
kati ya APR ya Rwanda na El Salam Wau ya Sudan Kusini wakati saa 10 kamili
jioni Yanga itaoneshana kazi na Atletico ya Burundi.
VIINGILIO MICHUANO YA
KAGAME 5,000/- KWA 2,000/-
Viingilio vya chini
katika mashindano ya Kombe la Kagame yanayoanza Jumamosi (Julai 14 mwaka huu)
vitakuwa sh. 5,000 kwa mechi za Yanga na Simba, na sh. 2,000 kwa mechi ambazo
hazihusishi timu hizo. Yanga ni bingwa mtetezi wakati Simba ni makamu bingwa
mtetezi.
Kwa upande wa mechi
zinazohusisha Yanga na Simba viingilio vitakuwa kama ifuatavyo; viti vya bluu
na kijani sh. 5,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 7,000, viti vya VIP C sh.
10,000, viti vya VIP B sh. 15,000 na viti vya VIP A ni sh. 20,000.
Siku ambazo Simba na
Yanga hazichezi, viingilio vitakuwa sh. 2,000 kwa viti vya rangi ya chungwa,
bluu na kijani, sh. 5,000 kwa viti vya VIP C, sh. 10,000 kwa viti vya VIP B na
sh. 15,000 kwa viti vya VIP A. Mshabiki akikata tiketi moja anaona mechi zote
mbili; mechi ya saa 8 na ile ya saa 10.
Timu za El Salam Wau
ya Sudan Kusini na Atletico ya Burundi zimewasili Dar es Salaam jana usiku
(Julai 11 mwaka huu) tayari kwa mashindano hayo wakati nyingine zote zilizobaki
kutoka nje zinawasili leo katika muda tofauti.
No comments:
Post a Comment