![]() |
Thom Saintfiet |
KOCHA wa klabu ya
Yanga, Mbelgiji Tom Saintfiet amemtema nahodha wa timu hiyo Shadrack Nsajigwa
katika kikosi chake cha wachezaji 20 ambacho kitakuwa kikitetea ubingwa wa
michuano ya Kombe la Afrika Mashariki na Kati maarufu kama Kombe la Kagame inayotarajiwa
kuanza kutimua vumbi Jumamosi.
Akizungumza na
waandishi wa habari mapema leo, kocha huyo amesema kuwa mbali ya Nsajigwa pia
amewaacha wachezaji watatu ambao wamo katika kikosi cha timu ya taifa ya vijana
chini ya miaka 20 ya Tanzania-Ngorongoro Heroes katika michezo ya hivi
karibuni inayowakabili.
Wachezaji hao
chipukizi ni Omega Seme, Simon Msuva na Frank Damayo ambao watakuwemo katika
kikosi cha Ngorongoro ambacho Jumamosi kitakuwa na mchezo wa kujipima nguvu
dhidi ya Rwanda na kurudiana nao tena Jumatatu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya
mchezo wa kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika dhidi ya Nigeria unaotarajiwa
kuchezwa Julai 29 mwaka huu.
Kocha huyo amesema
kuwa pamoja na kumtema Nsajigwa katika kikosi hicho lakini mchezaji huyo bado ni
muhimu katika timu hiyo na ameamua kumpa nafasi ya kujiweka fiti kwa ajili ya
msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambako atamtumia.
Kikosi kamili cha
Yanga ambacho kitashiriki Kagame kitakuwa na makipa Yaw Berko na Ally Mustafa
‘Barthez’, mabeki watakuwa Juma Abdul, David Luhende, Kelvin Yondani, Nadir
Haroub ‘Canavaro’, Godfrey Taita, Ladislaus Mbogo, Oscar Joshua na Stefano
Mwasika.
Wengine ni viungo
Athumani Iddi ‘Chuji’, Rashid Gumbo, Juma Seif ‘Kijiko’, Haruna Niyonzima,
Shamte Ally, Nizar Khalfan na Idrisa Assenga wakati washambuliaji watakuwa ni
Said Bahamuzi, Hamis Kiiza na Jerry Tegete.
Saintfiet amesema
kuwa kiungo Nurdin Bakari naye ametemwa katika kikosi hicho kutokana majeraha
yanayomsumbua ambapo daktari wa timu amesema ataweza kuwa fiti baada ya wiki
mbili wakati ambao michuano ya Kagame itakuwa tayari imeshaanza ndiyo sababu
kubwa ya kuachwa.
No comments:
Post a Comment