MTIHANI
WA MAWAKALA WA WACHEZAJI SEPT 27
Mtihani
kwa ajili ya watu wanaotaka kuwa mawakala wa wachezaji wanaotambuliwa na
Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) utafanyika Septemba 27 mwaka
huu saa 4 kamili asubuhi ofisi za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Kwa
wanaotaka uwakala huo wanatakiwa kujisajili ambapo watapewa kanuni mbalimbali
za FIFA na TFF ili waweze kujiandaa kikamilifu kwa mtihani huo utakaokuwa na
sehemu mbili. Sehemu ya kwanza ni maswali kutoka FIFA wakati nyingine ni kutoka
TFF. Ada ya mtihani ni dola 50 za Marekani.
Pia
Damas Ndumbaro na Ally Mleh wa Manyara Sports Management ambao tayari ni
mawakala wanaotambuliwa na FIFA wanatakiwa kufanya mtihani huo kama wanataka
kuendelea na uwakala kwa vile muda wa leseni zao za awali umemalizika.
Mawakala
wengine ambao ni John Ndumbaro, Mehdi Remtulla, Ally Saleh, Yusuf Bakhresa na
Said Tully leseni zao bado ziko hai.
SERENGETI
BOYS KUJIPIMA KWA ASHANTI
Timu
ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys) iliyokuwa
kambini kujiandaa kwa mechi dhidi ya Kenya itavunja rasmi kambi yake kesho
(Jumamosi) kwa mechi ya kirafiki dhidi ya Ashanti United.
Mechi
hiyo dhidi ya Ashanti United iliyoko daraja la kwanza itachezwa kuanzia saa 10
jioni Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam kwa kiingilio cha sh.
2,000.
Serengeti
Boys ilikuwa Septemba 9 mwaka huu icheze na Kenya kwenye mechi ya raundi ya
kwanza ya michuano ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, lakini Kenya
ikajitoa ambapo sasa itacheza na Misri katika raundi ya pili. Mechi ya kwanza
itachezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Mwishoni
mwa Septemba, Serengeti Boys itarejea tena kambini kujiandaa kuikabili Misri
ambapo kabla inatarajia kupata mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya timu
itakayotangazwa baadaye.
MCHEZAJI
WA MTIBWA SUGAR NAYE APATA ITC
Shirikisho
la Vyama vya Mpira wa Miguu Uganda (FUFA) limetuma Hati ya Uhamisho wa
Kimataifa (ITC) kwa ajili ya mchezaji Ayoub Hassan Isiko aliyejiunga na Mtibwa
Sugar akitokea timu ya Bull FC ya nchini humo.
ITC
hiyo ilitumwa jana (Agosti 30 mwaka huu), hivyo kufanya wachezaji ambao ITC
hazijapatikana hadi sasa kubaki wawili tu. Dirisha la usajili wa wachezaji
litafungwa rasmi Septemba 4 mwaka huu.
Wachezaji
ambao ITC zao bado hazijapatikana ni Salum Kinje na Pascal Ochieng kutoka AFC
Leopards ya Kenya waliojiunga na Simba. ITC hizo zinatarajiwa kupatikana wakati
wowote kwani tayari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limeshaziomba
kwa Shirikisho la Mpira wa Miguu Kenya (FKF) baada ya nyaraka zote zilizokuwa
zikitakiwa kupatikana.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment