Fainali za
michuano ya Airtel Rising Stars Afrika zimefikia tamati huku timu ya wavulana
ya Niger na wasichana kutoka Ghana zikishinda ubigwa wa michuano hiyo.
Niger
ilifunga Zambia 5-4 kwa mikwaju ya penati kushinda ubingwa wa kwanza wa
michuano ya Airetl Rising Stars 2012 kwa wavulana. Timu hizo zilimaliza dakika
90 ya mchezo bila ya kufungana licha ya kosa kosa nyingi kwa kila timu. Mchezo huo ulilazimika kuingia katika hatua ya penati baada ya kucheza dakika za nyongeza bila kufungana.
Niger
walishinda penati zao zote kupitia kwa Mamane Karibou, Issa Souleymane,
Abubacar Timbo, Idrissa Amadou na Issifou Garba. Timothy Sakala, Thomas Juma
Mutale, Dennis Chebuye na Albert Bwalya waliifungia Zambia huku Shadrack
Chimanya akikosa.
Kwa upande
wa fainali za wasichana, Ghana walitoka nyuma na kuifunga wenyeji Kenya
waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kushinda kwa 2-1. Kenya ndio waliokuwa wa
kwanza kufunga kupitia kwa Vivian Odhiambo dakika ya 27 kabla ya Emelia Lokko
kushawashisha dakika ya 43. Patience Narh ndio aliepeleka kilio kwa Wakenya kwa
kufunga bao la ushindi dakika ya 56.
Fainali hizo
zilihudhuriwa na nyota wa zamani wa Manchester United Peter Schmeichel ambaye
pia amechaguliwa kuwa balozi wa klabu hiyo hivi karibuni. Schmeichel ndio
aliekabidhi medali kwa washindi.
Michuano
hiyo ilikuwa ni moja ya mpango kambambe wa Airtel Rising Stars wenye nia ya kutafuta
na kukuza vipaji vya soka kuanzia ngazi ya chini. Kwa mwaka huu, michuano hiyo
ilishirikisha timu za vijana 18,000 na wachezaji 324,000 kutoka nchi 15. Pia
michuano ya mwaka ilikuwa ya aina yake kwani imeweza pia kushirikisha
wasichana.
Jumla ya wachezaji
432 walikuwa Nairobi kwa wiki nzima shukrani kwa kampuni ya simu za mikononi ya
Airtel. Vijana hao walionyesha vipaji vya hali ya juu na ni wazi kwamba mpira
wa Afrika unaelekea mahali pazuri.
Timu za
Niger na Ghana zilizawadiwa fedha taslimu dola10,000 kila moja kwa kuwa bingwa.
Pia timu hizo zitapata fursa kwa wachezaji wake wote kushiriki kliniki maalum
chini ya waalimu wa mpira wa miguu kutoka klabu za Arsenal na Manchester United
za nchini Uingereza. Kliniki hiyo itafanyika Nairobi, Kenya na Accra Ghana.
No comments:
Post a Comment