MUDA WA MECHI ZA ‘LIVE’ SUPER WEEKEND
Mechi
tano za Ligi Kuu ya Vodacom za Super Weekend katika mzunguko wa kwanza
zitakazooneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha Super Sport
zitaanza kati ya saa 1-.30 jioni na saa 1 kamili usiku.
Septemba
28 mwaka huu kutakuwa na mechi kati ya Azam na JKT Ruvu itakayofanyika
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 1 kamili usiku. Mechi ya
Simba na Tanzania Prisons itakayochezwa Septemba 29 mwaka huu Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam itaanza saa 11 kamili jioni.
Yanga
na African Lyon zenyewe zitapambana Septemba 30 mwaka huu Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 11 kamili jioni wakati Ruvu Shooting na
Mtibwa Sugar zitaoneshana kazi Oktoba 1 mwaka huu Uwanja wa Azam
Complex, Dar es Salaam kuanzia saa 10.30 jioni.
Mechi
ya mwisho katika Super Weekend itakuwa Oktoba 3 mwaka huu Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam ikiwakutanisha watani wa jadi Yanga na Simba, na
itaanza kutimua vumbi saa 1 kamili usiku.
TWFA YATANGAZA KAMATI YA UCHAGUZI
Chama
cha Mpira wa Miguu wa Wanawake Tanzania (TWFA) kimetangaza Kamati ya
Uchaguzi yenye wajumbe watano kwa ajili ya uchaguzi wake unaotarajiwa
kufanyika Novemba mwaka huu.
Kaimu
Mwenyekiti wa TWFA, Margreth Mtaki amewaambia Waandishi wa Habari, Dar
es Salaam leo kuwa kamati hiyo itaongozwa na Ombeni Zavala, na itarajia
kutangaza mchakato wa uchaguzi huo Jumatatu (Septemba 24 mwaka huu).
Aliwataja
wajumbe wengine wa kamati hiyo yenye jukumu la kuendesha uchaguzi wa
chama hicho kuwa ni Rachel Masamu, Lloyd Nchunga, Nancy Mabula na Maneno
Tamba.
Pia
aliwataka wadau wa mpira wa miguu wa wanawake kujitokeza kugombea
nafasi mbalimbali za uongozi katika TWFA mara Kamati ya Uchaguzi
itakapoanza mchakato.
Wakati huo huo,
uchaguzi wa vyama vya mpira wa miguu vya mikoa ya Kilimanjaro (KRFA) na
Manyara (MARFA) unafanyika kesho (Septemba 22 mwaka huu).
No comments:
Post a Comment