Katibu wa TASWA Amir Mhando. |
CHAMA Cha Waandishi wa Habari za
Michezo Tanzania (TASWA), kimeanza mchakato wa Tuzo kwa Wanamichezo Bora wa
Tanzania mwaka 2012.
Kama ilivyokuwa mwaka uliopita Kamati ya
Utendaji ya TASWA imeamua suala la mchakato wa kuwapata wanamichezo hao
lifanywe na kamati maalum nje ya Kamati ya Utendaji ya TASWA lengo ikiwa ni
kupanua wigo na kuwashirikisha wadau wengi zaidi katika jambo hili nyeti.
Jukumu
la Kamati ya Utendaji ya TASWA itakuwa ni kuhangaika na mambo ya
wadhamini na masuala mengine yahusuyo sherehe hizo ambazo tunataka ziwe
za aina yake.
Kutokana na hali hiyo Kamati ya Utendaji ya
TASWA iliyokutana wiki iliyopita iliteua kamati maalum ya watu 11 kusimamia mchakato
wa kuwapata wanamichezo hao, ambapo kamati hiyo inayotarajia kuanza vikao vyake
Jumatano Januari 30, 2013 itakuwa chini ya uenyekiti wa mwanachama wa TASWA,
Haji Manara.
Kamati ya Utendaji imemkabidhi jukumu
Manara baada ya kujiridhisha pasi na shaka uzoefu wake katika masuala ya
michezo na pia uzoefu wake katika mambo mbalimbali ya kiutawala, hivyo kuwa na
imani kwamba ataendesha vizuri mchakato kama walivyofanya watangulizi wake.
Wajumbe saba wa kamati hiyo wanatoka nje ya
Kamati ya Utendaji ya TASWA ambao ni Jane John, Dina Ismail, Jabir
Idrissa, Tulo Chambo, Abdallah Mweri na ofisa
mmoja ambaye ataombwa kutoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT), wakati wajumbe
wanne wanatoka Kamati ya Utendaji ya TASWA ambao ni Grace Hoka, Zena Chande,
Alfred Lucas na Amir Mhando.
No comments:
Post a Comment