Ilkay Gundogan |
Kocha Mkuu wa Manchester United ya England,
David Moyes amesema angependa kusajili baadhi ya wachezaji kuimarisha
kikosi chake lakini ana wasi wasi huenda asiweze kuwapata wachezaji hao
katika usajili wa dirisha dogo mwezi huu wa Januari.
Kiungo Marouane Fellaini ndiye mchezaji pekee
aliyesajiliwa tangu kuwasili kwa David Moyes katika kikosi cha
Manchester United kinachoshikilia nafasi ya saba kwenye msimamo wa ligi
kuu ya Kandanda ya England inayoendelea.
Kocha huyo amenukuliwa akisema kuwa
"Tungependa kuongeza wachezaji lakini swali la kujiuliza,ni Je wanaweza
kupatikana wachezaji hao"?
Akizungumza Jumapili ya jana baada ya kichapo cha mabao
2-1 dhidi ya Swansea kwenye kombe la FA, Kocha huyo amekiri kuwa kuna
mahitaji makubwa ya wachezaji wapya ndani ya kikosi cha Manchester
United, lakini hakuna umuhimu wa kutangaza jambo hilo kwa sababu
wachezaji ambao angependa kuwasajili hawawezi kupatikana katika usajili
wa dirisha dogo mwezi Januari.
Kocha huyo amekiri kuwepo kwa hali ya wasi wasi
klabuni hapo msimu huu baada ya timu ya Manchester United kupoteza mechi
nne kati ya sita zilizochezwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Old Traford.
Kichapo cha Jumapili cha mabao 2-1 dhidi Swansea
kilikuwa cha pili katika kipindi cha miaka thelathini kwa Manchester
United kuondolewa katika raundi ya tatu ya michuano ya Kombe la FA, huku
mwanasoka Wilfried Bonny akitia kambani bao la ushindi katika dakika ya
90, ushindi ambao ulikuwa wa kwanza kwa Swansea katika uwanja wa Old
Traford,baada ya Javier Hernandes kusawazisha bao la kuongoza la Swansea
lililotiwa kimiani mapema na Wayne Routledge.
Kipigo cha Jumapili dhidi ya Swansea ambacho ni
cha saba katika michuano yote kwa ujumla msimu huu kimekuja kikifuatia
kingine ambacho Manchester United ilikipata siku ya mwaka mpya baada ya
kupigwa na Tottenham Hostspurs mabao 2-1.
Akizungumzia kipigo hicho kiungo Darren Fletcher
amesema kuwa wachezaji wa Manchester waliwaangusha mashabiki na kocha
wao huku akielezea kuwa hali hiyo imeleta maumivu na hasira kubwa kutoka
kwa mashabiki wa timu hiyo kufuatia mwenendo wa timu nzima msimu huu
ambapo imepoteza mechi nne kati ya sita zilizochezwa katika uwanja wa
nyumbani wa Old Traford.
No comments:
Post a Comment