Rais mpya wa kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach amesema hali ni
shwari mjini Sochi katika maandalizi ya kufunguliwa rasmi michezo ya
Olimpiki ya majira ya baridi leo (07.02.2014) mjini humo.
Kamati ya Olimpiki ya Kimataifa imefanya mkutano wake wa kwanza leo na
waandaaji wote wa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi, ili
kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama kilivyopangwa.
Rais mpya wa kamati hiyo Thomas Bach, amesema kawaida ya kila ufunguzi wa
michezo ya aina yoyote hakukosekani matatizo ya hapa na pale lakini
kila kitu kwa sasa kinaendelea salama. Hata hivyo Bach hakueleza zaidi
juu ya matatizo hayo.
Bach amesema anamatumaini makubwa kuwa ufunguzi unjaotarajiwa kufanyika
leo jioni utafana na michezo hiyo ya Olimpiki ya msimu wa baridi itakuwa
ya mafanikio.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon na Rais mpya wa kamati ya Kimataifa ya Olimpiki Thomas Bach
Katika ufunguzi huo wanamuziki mashuhuri wa mtindo wa Pop
nchini Urusi wanaojulikana kama tATu watashiriki kwa kuimba wimbo juu ya
wasichana wawili wa shule walioko kwenye uhusiano wa kimapenzi.
Wimbo huo kwa jina "Not Gonna Get Us" yani hamutotupata umenuiwa
kuonesha sura ya Urusi mbele ya macho ya ulimwengu kama ambavyo
wanaharakati, na viongozi wa dunia wanavyoipinga sheria ya taifa hilo
dhidi ya watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja.
Mmoja wa watayarishaji wa sherehe za leo Konstantin Ernst amesema
wamechagua wimbo huo "Not Gonna Get Us" kwa kuwa ndio wimbo pekee nchini
Urusi unaoweza kutambulika kimataifa.
Shaka ya Ufanisi wa Michezo ya Sochi
Haki za mashoga, kukandamizwa kwa wanaharakati wa haki za binaadamu,
uharibifu wa mazingira, ufisadi wa hali ya juu, hali duni za wafanyakazi
na wajenzi wa eneo la michezo hiyo na hatua kali za ulinzi, haya yote
yametilia shaka kufanikishwa kwa Michezo hiyo.
Huku hayo yakiarifiwa rais wa China Xi Jinping alionya juu ya
kuingiza siasa katika michezo hiyo. Vyombo vya habari nchini humo
vimesema hatua hiyo ni ya kumuunga mkono rais Vladimir Putin wa Urusi,
kabla ya kuanza rasmi michezo hiyo ya olimpiki ya msimu wa baridi.
Viongozi hao wawili walikutana hapo jana mjini Sochi katika ziara ambayo
inapishana na ziara ya Waziri mkuu wa Japan Shinzo Abe ambayo huenda
ikadhoofisha zaidi mahusiano ya nchi hiyo na China juu ya udhibiti wa
visiwa fulani.
Baadhi ya Viongozi kutohudhuria Michezo
Licha ya hayo kuna wasiwasi juu ya kuyumba kwa usalama katika ufunguzi
wa michezo hiyo, kutokana na hilo rais Putin ameamrisha mikakati maalum
ya usalama kuwekwa nchini kote hasa baada ya kuuwawa watu 34 katika
shambulizi la bomu mjini Volgograd mwezi Desemba, mwaka jana.
Ulinzi umeimarishwa nchini humo hasa mjini Sochi huku vikosi
vikiwa katika tahadhari ya hali ya juu kufuatia kitisho cha kutokea
mashambulizi ya kigaidi yanayodaiwa kupangwa na waislamu walio na
itikadi kali.
Marekani kwa upande wake inahofu juu ya usalama katika michezo hiyo.
Rais wa Marekani Barrack Obama, Francois Hollande wa Ufaransa, Waziri
Mkuu wa Uingereza David Cameron na rais wa Ujerumani Joachim Gauck
hawatahudhuria michezo hiyo.
No comments:
Post a Comment