Ufunguzi wa michezo ya olimpiki ya majira ya baridi mjini Sochi
ulifanyika jana Ijumaa(07.02.2014) kwa tamasha kubwa la kuvutia
lililoshuhudiwa na rais Vladimir Putin wa Urusi.
Rais Putin amelenga kutuliza hofu za mashambulizi ya kijeshi na pia
kuondoa mzozo kuhusiana na haki za mashoga , hali iliyotia doa wakati
mashindano hayo yanakaribia kuanza.
Putin ameimarisha hadhi yake kwa nchi yake kuwa mwenyeji wa mashindano
salama na ya mafanikio ya olimpiki katika mji wa kitalii katika bahari
nyeusi wa Sochi, ambako tamasha la ufunguzi lililokuwa na kila aina ya
shamra shamra katika uwanja uliosheheni watazamaji 40,000 katika uwanja
mpya wa Fisht uliashiria mwanzo wa mashindano hayo kwa ukamilifu.
"Natangaza mashindano haya ya 22 kuwa yamefunguliwa" amesema Putin
akifungua rasmi tukio hilo ambalo anatarajia kuwa litasafisha heba yake
pamoja na nchi yake duniani. Rais wa kamati ya kimataifa ya olimpiki
Thomas Bach amesema haya yatakuwa mashindano ya kuvutia.
"Kuna hamasa kubwa na nina matarajio mwenge wa olimpiki ukiwaka katika
uwanja wa olimpiki, hata wanamichezo watakuwa katika hali kama hiyo na
nina hakika litakuwa tamasha la kufurahisha."
Gharama za mashindano
Watayarishaji wametetea gharama za kuendesha mashindano hayo ya Sochi
huku kukiwa na wasi wasi kutoka kwa maafisa wa olimpiki kuwa gharama
kubwa huenda ikawaweka wadhamini kando katika mashindano yajayo.
Licha ya manung'uniko ya hapa na pale kuhusu maeneo ya malazi ambayo
hayakukamilika katika sehemu kadha , hali miongoni wa washiriki wa
mashindano hayo pamoja na maafisa wao baada ya michezo kadha ya mwanzo
mjini Sochi imekuwa ya matumaini.
Michezo hiyo imeanza kwa wanamichezo kushindana katika michezo mbali mbali.
Mwanariadha wa Marekani Sage Kotsenburg amekuwa
mwanariadha wa kwanza kunyakua medali ya kwanza ya dhahabu katika
michezo ya Olimpiki ya Majira ya Baridi huko Sochi
nchini Urusi.
Sage Kotsenburg, amenyakua medali hiyo katika
mchezo wa kuteteleza katika barafu kwa kwa kutumia ubao kwa upande wa
wanaume, ukiwa ni mmoja katika michezo 12 mipya iliyoingizwa katika
michuano hiyo, ili kuwavutia vijana.
Mwanamke wa kwanza kushinda medali
ya dhahabu ni Marit Bjoergen wa Norway,katika mbio za marathon za
kilomita 15. Umati mkubwa wa mashabiki wa Uholanzi wanatarajiwa
kumshangilia bingwa mtetezi wa mchezo wa kuteleza katika barafu, Sven
Kramer, akijaribu kutetea taji lake kwa upande wa wanaume mita elfu
tano.
Rais Vladmir Putin wa Urusi alifungua rasmi
jana(Ijumaa), mashindano ya Olimpiki ya majira ya baridi katika mji wa
utalii wa Sochi katika sherehe zilizofana.
Waliokuwa wanariadha mashuhuri nchini Urusi
waliubeba mwenge wa Olimpiki kabla ya kuwashwa na aliyekuwa mlinda lango
wa mchezo wa magongo Vladislav Tretiak pamoja na mchoraji wa barafu
Irina Rodnina.
Katika siku 16 zijazo,karibia wanariadha 3000
watashiriki katika michezo mbalimbali 98 katika mashindano hayo
yaliodaiwa kugharimu takriban dola billioni 50.
Bundesliga
Son Hueng Min wa Leverkusen akifurahia bao lake |
Na katika kandanda, ligi ya Bundesliga imeingia katika mchezo wake wa 20
jana Ijumaa wakati Bayer Leverkusen ilifanikiwa kushinda mchezo wa
kwanza kwa bao 1-0 dhidi ya Borussia Moenchengladbach na kuendeleza
vipigo dhidi ya timu hiyo iliyokuwa ikicheza nyumbani.
Katika mchezo huo ambao haukuwa na mvuto wa kutosha na nafasi chache za
kufunga Son Heung Min alidhihirisha kuwa ni mmoja kati ya wachezaji
ambao wanaweza kubadili matokeo na kupachika bao pekee usiku huo katika
dakika ya 62 ya mchezo.
Leo VFL Wolfsburg inaikaribisha Mainz , wakati Bremen inakibarua na
Borussia Dortmund. Pambanoi la watani wa jadi linafanyika huko mkoani
Bavaria ambapo Nürnberg inatiana kifuani na miamba wa Bundesliga Bayern
Munich.
Alipoulizwa kuhusu pambano hilo kocha wa Bayern Pep Guardiola amesema
lolote linaweza kutokea, kwani pambano la watani wa jadi mara zote
halitabiriki. Lakini amesisitiza kuwa kikosi chake kinataka kuhakikisha
kuwa hakipotezi mchezo.
Freiburg inamiadi na Hoffenheim , Eintracht Frankfurt inaikaribisha
Eintracht Braunschweig , wakati Hamburg itaoneshana kazi na Hertha BSC
Berlin.
Kesho Jumapili (09.02.2014) ni zamu ya Stuttgart kuoneshana kazi na Augsburg na Schalke wanaikaribisha Hannover nyumbani.
No comments:
Post a Comment