Nahodha wa timu ya taifa ya mchezo wa tennis katika kombe la Davis, Carsten Arriens amezomewa na mashabiki wa nyumbani
mjini Frankfurt jana Jumapili licha ya kuiongoza timu yake katika
ushindi mnono wa 4-1 dhidi ya mabingwa mara tano wa kombe hilo
Uhispania.
Sababu ya mashabiki kuchukua hatua hiyo ni kutokana na wachezaji maarufu
wa tennis wa Ujerumani kujitoa katika kinyang'anyiro hicho kutokana na
sababu mbali mbali.
Hii ilikuwa na maana kwamba mashabiki waliolipa kiasi cha euro 65 kuona
mapambano ya wachezaji wawili wawili waliona pambano moja tu ambalo
halikuwa na msisimko wowote, kati ya Daniel Brands na Roberto Bautista
Agut wa Uhispania.
Michuano ya Olimpiki
Katika michuano ya Olimpiki ya Sochi, Rais wa kamati ya olimpiki ya
Kimataifa IOC Thomas Bach amesema usalama wa kutosha na ukosoaji wa
Urusi kuhusu sheria ya kupinga ushoga havitachafua michezo hiyo ya
Olimpiki mjini Sochi.
Bach pia amerudia utetezi wake kuhusu matumizi ya fedha ya Urusi katika michezo
hiyo , akisema kuwa fedha hizo zinakwenda katika kufanyia mageuzi ya
muda mrefu katika eneo hilo. Akizungumza na waandishi habari siku nne
kabla ya ufunguzi wa michezo hiyo, Bach ameeleza matumaini yake kwa
uwezo wa Urusi kuweza kutoa ulinzi kwa michezo hiyo huku kukiwa na
kitisho cha mashambulizi ya kigaidi kutoka kwa wapiganaji wa eneo la
kaskazini mwa eneo la Kaukasus.
No comments:
Post a Comment