Kipindi cha usajili wa wachezaji wapya, kimefikia tamati na kuna wale
waliofaidika na wale walioachwa wakijikuna vichwa. Katika ligi
Ujerumani, timu iliyohitaji sana wachezaji wapya ni Borussia Dortmund.
Dortmund kwa sasa inakabiliwa na matatizo chungu nzima kutokana na idadi
ya wachezaji wake waliopata majeraha. Imebidi vijana hao wa njano
wamsajili kiungo Mserbia Milos Jojic. Usajili wa Jojic aliyehamia
Dortmund kutoka Partizan Belgrade na usajili wa Mpoland Ludovic Obraniak
katika klabu ya Werder Bremen kutoka Girondins Bordeaux ndio shughuli
pekee iliyofanywa katika dakika za mwisho mwisho wakati kipindi cha
usajili wa wachezaji cha Januari kilipofikia kikomo jana. Kwa jumla,
katika kipindi hiki, timu 18 za Bundesliga ziliwasajili wachezaji 32 na
kuwauza 37. usajili mkubwa ni wa Mbelgiji Kevin De Bruyne aliyejiunga na
VfL Wolfsburg kutoka Chelsea kwa kiasi cha euro milioni 20. Mkorea
Kusini Koo Ja-Cheol alihama Wolfsburg na kujiunga na Mainz kwa kiasi cha
euro milioni tano.
Schalke ilimtuma kiungo Mmarekani Jermaine Jones katika klabu
ya Besiktas ya Uturuki kwa mkopo wakati nao miamba Bayern wakitosheka na
kikosi chao…ijapokuwa walimwacha beki wao Jan Kirchoff akajiunga na
Schalke kwa mkopo.
Tukiwachana na mambo ya uhamisho wa wachezaji, sasa tuangalia ligi iko
vipi? Na suali kuu linaloulizwa na kila shabiki ni, nani anayeweza
kuipunguza kasi ya Bayern Munich?
Huenda wanaongoza msimamo wa ligi na pengo la pointi 13 dhidi ya nambari
mbili, na wamecheza mechi 43 mfululizo bila kushindwa, lakini kocha wa
Bayern Munich Pep Guardiola ameionya timu yake kusalia makini. Miamba
hao wa Bavaria wanawaalika Eintracht Frankfurt kesho Jumapili katika
uwanja wa nyumbani Allianz Arena huku wachezaji Arjen Robben na Frank
Ribery wakirejea kikosini baada ya kupona majeraha ya miguu.
Guardiola ametoa onyo hilo kuafuatia mchuano wa wiki wiki iliyopita
ambao walitokwa jasho kwa kushinda magoli mawili kwa moja dhidi ya
Stuttgart. Bayer Leverkusen na Borussia Dortmund zimekiri kuwa
zinapigania nafasi ya pili tu kwa sababu tayari taji la ligi
limewaponyoka. Leverkusen wanawaalika Stuttgart hii leo. Nambari nne
Borussia Moenchengladbach ambao wana pointi sawa na Dortmund wanacheza
leo dhidi ya Hanover.
Katika mechi nyingine za leo, Schalke 04 v VfL Wolfsburg, Hoffenheim v
Hamburg, Mainz v Freiburg, Augsburg v Werder Bremen. Kesho Jumapili,
Hertha Berlin watafunga kazi dhidi ya Nuremberg.
No comments:
Post a Comment