Hicho ndicho kilikuwa kichapo kikubwa zaidi katika historia yao ya miaka
100 ya soka. Huku mchezaji wao nyota Neymar akikosekana kwa sababu ya
jeraha, kila mmoja nchini Brazil alifahamu kuwa ungekuwa mtihani mkubwa
kwao dhidi ya Ujerumani. Hakuna aliyetarajia matokeo ya jana. Bila shaka
pengo la Thiago Silva pia lilikuwa kubwa mno na waliotwikwa mzigo wa
kuliziba yaani Dante na David Luiz, walizidiwa maarifa.
Miaka 64 baada ya Brazil kutumbukia katika maombolezi ya kitaifa
kufuatia kichapo walichopata katika fainali ya mwaka wa 1950, wenyeji
walibomolewa katika kichapo ambacho kinaweza kuwapa msongo wa akili
kuliko hata kile cha “Maracanazo”.
Nahodha wa Brazil David Luiz, huku akitiririkwa na machozi, maramoja
aliomba radhi kwa taifa baada ya kipigo hicho. Kocha wake Luiz Felipe
Scolari aliyeonekana kupatwa na mshangao mkubwa, aliyaunga mkono
matamshi hayo akiwataka wananchi wawasamehe kutokana na makosa
waliyofanya. Rais Dilma Roussef pia alituma ujumbe wa kuituliza mioyo ya
mashabiki.
Thomas Müller ambaye alifunga goli lake la tano katika dimba hili,
alisema hawakuamini matokeo hayo ya kushangaza. Tikiti ya Ujerumani
kuelekea mjini Rio ilipatikana baada y akipindi cha kwanza cha
maangamizi ambacho walifunga magoli manne katika dakika sita.
Müller alifungua ukurasa wa mabao katika dakika ya 11 kutokana na mkwaju
wa kona. Miroslav Klose kisha akatia kimyani la pili katika dakika ya
23 – ambalo lilikuwa lake la 16 na kumfanya kuwa mfungaji wa magoli
mengi katika historia ya Kombe la Dunia.
Kisha milango ya magoli ikafunguka. Toni Kroos alifunga mara mbili
katika dakika ya 24 na 26 ili kufanya mambo kuwa 4-0 na kisha Sami
Khedira akabusu wavu na kufikisha 5-0 katika dakika ya 29.
Huku wakiwa wamekufa na kuzikwa katika kipindi cha nusu saa, umati
katika uwanja wa Mineirao ulibaki kimya kama maji mtungini. Mashabiki
wengi walibubujikwa machozi huku wakijaribu kung'amua kilichokuwa
kikitendeka uwanjani. Baada ya goli la tano, hata kabla ya kukamilika
kipindi cha kwanza, mamia ya watu waliacha viti vyao na kuondoka.
Katika kipindi cha pili, Brazil ilianza kwa kishindi lakini mateso
yaliendeela katika dakika ya 69 wakati Andre Schuerrle alipopachika
wavuni goli. Schuerrle kisha akafunga lake la pili katika dakiak ya 79
na kufanya mambo kuwa 7-0. Goli hilo liliwafurahisha mashabiki na hata
Wabrazil waliinuka na kumpongeza Schuerrle kutokana na maarifa na ujuzi
aliotumia. Mara ya mwisho kupata kichapo cha aina hiyo ilikuwa mwaka wa
1920 walipozabwa magoli 6-0 na Uruguay.
Goli la dakika ya mwisho lake Oscar la kufutia machozi hata
halikuwatikisa mashabiki wa Brazil ndani ya uwanja. Kocha wa Ujerumani
Joachim Löw amesema Brazil walishtuka baada ya kufunwga magoli ya
mapema, kwa sababu hawakutarajia hilo. Hawakujua wafanye nini. Safu yao
ya ulinzi haikuwa imejipanga. Ujerumani sasa wanajiandaa kwa fainali
itakayochezwa katika uwanja wa Maracana Jumapili tarehe 13. Na mpinzani
wao atajulikana leo, kati ya Argentina na Uholanzi ambao wanakutana
katika nusu fainali ya pili.
No comments:
Post a Comment