KWA MAWASILIANO ZAIDI TUMIA BARUA PEPE rockersports212@yahoo.com AU TUPIGIE KUPITIA NAMBARI 0767166607 AU 0717166607. KARIBU SANA. 66666666607 AU 0717166607

Saturday, February 16, 2013

WACHEZAJI WA AZAM NA AHADI YA USHINDI HII LEO (Source Azam website)

  Kuelekea kwenye mchezo wake wa kwanza katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Nasri Juba ya Sudan Kusini, wachezaji wa Azam FC kwa pamoja wamesema wamejiandaa kikamilifu kucheza mchezo huo.
 
Azam FC itacheza na Al Nasri Juba kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, hii ni mara ya kwanza kwa Azam FC kushiriki mashindano makubwa yanayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF).
  Kwa nyakati tofauti www.azamfc.co.tzimepata fursa ya kuwasikia wachezaji wa Azam FC wakieleza furaha yao kwa timu kupata nafasi hiyo pia wamezungumzia maandalizi waliyofanya na yanayowapa matumaini ya kushinda katika mchezo huo.
 
John Bocco.
Mshambuliaji wa Azam FC, na ni mmoja kati ya wachezaji  waliopanda na timu hiyo tangu ikiwa ligi daraja la kwanza, anasema ni faraja na furaha kwake kufikia mafanikio hayo ambayo sio kwa klabu tu pia ni mafanikio kwake.
  Anasema yeye pamoja na wachezaji wenzake wamejiandaa kufanya vizuri katika mchezo huo, kikubwa ni kujituma kwa wachezaji wenzake pamoja na kuwa na umoja watashinda mchezo huo.
  "Nimefurahi kupata mafanikio hayo nikiwa mmoja wa waliochangia, kwetu itakuwa mechi ngumu lakini tunaamini kwa maandalizi haya tuliyopata ushindi lazima" anasema Bocco.
 
Mwadini Ally
Golikipa namba moja wa Azam FC anasema anaimani watafanya vizuri katika mchezo, wamepata maandalizi imara na ya kutosha.
  “Tumejiandaa, utakuwa mchezo wa aina tofauti lakini tunaamini tutafanya vizuri, kikubwa tunaomba uzima na Mungu atusaidie kwa uwezo wake tutafanikiwa” anasema Mwadini.
 
Khamis Mcha Viali
Kiungo wa Azam FC anasema mashindano hayo hayana timu nyepesi kila timu ni ngumu, kwa kujua hilo wamejipanga vizuri kupambana na wapinzani wao Al Nasri Juba.
  “Tumejipanga vizuri na kila mchezaji anahamu ya kucheza mchezo huo, tutafanya vizuri tukiwa kama wawakilishi wanchi kwetu ni faraja na hatutawaangusha” anasema Mcha.
 
Salum Abubakar 'Sure Boy'
Kiungo mahiri wa Azam FC naye alikuwa mmoja wapo wa waliopanda na timu anasema mchezo huo utakuwa mgumu  kwa kuwa ndo wanaanza, itawapa shida mwanzoni lakini watajitahidi wapate matokeo mazuri.
  "Kwanza furaha niliyo nayo siwezi kuielezea, kuipandisha timu ikafanya vizuri kwenye ligi na sasa tupo kimataifa, nasubiri muda ufike, tumejiandaa mimi na wenzangu kufanya vizuri" anasema Sure Boy.
  Sure anasema mbali na furaha bali ni changamoto pia kwake ambayo wanatakiwa wafanye vizuri ili kupata nafasi nyinge ya kucheza kombe kubwa zaidi ya hilo.
 
Waziri Salum
Beki wa pembeni wa Azam FC anasema kila mchezaji yupo sawa kwa ajili ya mechi hiyo wanasubiri muda ufike waingie kupambana kwa kuwa wamejiandaa kikamilifu.
  “Tutaendeleza ushindi kama tulivyoanza kwenye ligi, naamini sisi tupo vizuri kila idara kikubwa tuombe uzima tu kila kitu kitakuwa sawa” anasema Waziri.
 
Ibrahim Mwaipopo
Mchezaji wa muda mrefu katika kikosi hicho, hii itakuwa mara yake ya kwanza kucheza mashindano hayo anasema wamepata maandalizi mazuri kutoka kwa kocha anaamini watashinda.
  Anasema kuwepo wachezaji wenye uzoefu na mashindano ya kimataifa ni sehemu ya kuamini kuwa watafanya vizuri, matarajio yake kuona timu yake ikivuka hatua katika mashindano hayo.
  Kiungo huyo anasema mechi za kirafiki, mazoezi wanayopata yameiunga vizuri timu hiyo mfano ni kuanza vizuri mzungo wa pili wa ligi.
 
Abdi Kassim ‘Babi’
Kiungo wa Azam FC mwenye uzoefu wa kutosha kwenye mashindano ya kimataifa anasema wamejiandaa vizuri kwa kuwa timu inaundwa na wachezaji wengi wenye uzoefu ambao anaamini watasaidia kuipa mafanikio zaidi.
  “Tumejiandaa na tunajiamini kufanya vizuri kikubwa tunawaomba Watanzania na mashabiki wetu watupe supoti ya kutosha sisi tutafanya vizuri” anasema Babi.
 
Gaudence Mwaikimba
Mshambuliaji wa Azam FC anasema kutokana na maandalizi waliyofanya zikiwepo mechi nyingi za kirafiki anaamini watapata matokeo mazuri katika mechi hiyo.
  “Tumepata uzoefu wa kutosha kwa kuwa tumecheza mechi za kirafiki Congo, Zanzibar, Kenya na mechi za ligi, tunaomba kila mchezaji aamke salama ili tufanikishe lengo letu ambalo ni ushindi” anasema Mwaikimba.
 
Himid Mao
Mchezaji amejiunga na klabu hiyo kuanzia akiwa mdogo  (Azam Academy) anasema kuingia katika mashindano hayo ni kuweka historia nzuri ya mafanikio kwa klabu na kwake pia kama mchezaji aliyechangia mafanikio hayo.
  "Ni mechi ya kihistoria, nimekuwa na klabu tangu nikiwa nacheza U20, nashindwa kujizuia furaha yangu lakini naelekeza kufakisha ushindi katika mchezo huo" anasema Himid.
 
Aishi Salum Manula
Golikipa namba mbili wa Azam FC anasema kupata nafasi hiyo ni furaha kwake na ni changamoto inayowataka kufanya vizuri, hivyo wamejiandaa vizuri kupambana katika mchezo wao na Al Nasri Juba na watafanya vzuri.
  “Tuna matumaini makubwa ya kufanya vizuri, tutatumia mchezo huu wa nyumbani kupata matokeo mazuri yatakayotuweka katika nafasi ya kuingia hatua ya pili, watanzania wazidi kutuombea” anasema Aishi.
 
Samih Haji Nuhu
Beki wa pembeni atakayekosa mechi mbili za mwanzo anasema kwake ni furaha timu inacheza mashindano hayo anaamini ushindi utapatikana kutokana na maandalizi wanayopata.
  “Tumejipanga vizuri zaidi, tuna matumaini ya kila mmoja kushinda na tunategemea kupata matokeo mazuri kama tulivyopanga” anasema Haji.
 
Tchetche Kipre na Michael Bolou
Wachezaji wa kigeni ambao ni mapacha  kutoka nchini Ivory Coast wanasema utakuwa mchezo mgumu na wenye ushindani kwa kuwa hawaifahamu timu watakayocheza nayo hivyo watatakiwa kuwa makini zaidi.
  Kulingana na maandalizi, timu iko tayari kucheza na klabu yoyote ile kwa sasa na wanaamini kushinda katika mchezo wa leo ni sehemu ya mipango yao.
  "Hii ni kama michezo mingine tatizo tu hatuwafahamu wapinzani wetu, hiyo haitukatisha tamaa tutapigana muda wote na kupata matokeo mazuri" anasema Kipre.
 
Malika Ndeule
Hii itakuwa mechi yake ya kwanza kucheza kombe la Shirikisho Afrika anasema wamejiandaa vizuri na watatumia vizuri uwanja wa nyumbani kupata ushindi.
  “Tunacheza nyumbani kwetu matokeo ya ushindi ndio nia yetu ambayo itatuweka vizuri katika mchezo wa marajeano ambao utakuwa ugenini” anasema Malika
 
Jabir Aziz
Kiungo wa Azam FC mwenye uzoefu na mashindano ya kimataifa anasema mechi za kimataifa zinakuwa na sura tofauti, mara nyingi huwa ngumu na zenye ushindani lakini kwa upande wao wamejiandaa kwa kila kitu.
  Anasema mafunzo wanayopata kutoka kwa kocha Stewart Hall anaamini yataiwezesha timu hiyo kuvuka na kusonga mbele katika hatua nyingine.
 
Jockins Atudo
Beki wa Azam FC raia wa Kenya anasema mchezo utakuwa sawa na michezo mingine kwa kuwa wamepata matayarisho mazuri.
  “Sisi hatuna wasiwasi, tumejitayarisha vizuri kwa mchezo huo, tunawahakikishia ushindi mashibiki wetu popote walipo” anasema Atudo.
 
Seif Abdalah ‘Karihe’
Mchezaji wa Azam FC anayeshiriki kwa mara ya kwanza mashindano ya CAF anasema wamejiandaa wanatakiwa kuongeza umakini zaidi ili kufanikisha malengo yao ya kupata ushindi.
  “Tukiongeza umakini tutatapata matokeo mazuri nyumbani na kurahisisha kazi katika mchezo wa pili, hayo ndio malengo ya kila mmoja wetu” anasema Karihe
 
Humphrey Mieno
  Kiungo mpya amesajiliwa kutoka nchini Kenya anasema kila mchezaji yupo katika hari nzuri na wanahamu ya kucheza mchezo huo hivyo ushindi utakuwepo,
  Anasema watapata matokeo mazuri kutokana na maandalizi mazuri wanayapata tangu mwanzo
 
Brian Umony
Mshambuliaji wa Azam FC kutoka nchini Uganda anasema ni mechi muhimu kwao wanacheza nyumbani hivyo wanatakiwa kupata magoli mengi yatakayowaweka katika nafasi nzuri.
  “Tuna faida ya kucheza nyumbani ni wakati wetu wa kufunga magoli mengi zaidi hii itatusaidia katika mchezo wetu wa marudiano kwa kuwa kucheza ugenini kuna ugumu mkubwa” anasema Umony.
 
 
Abdulhalim Humud
Mchezaji wa Azam FC mwenye uzoefu na mashindano ya kimataifa anasema ni mechi muhimu kwao kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa klabu, wanaiona mechi hiyo kama fainali hivyo watapambana muda wote wa mchezo.
  Anasema watatumia nafasi hiyo kuwaonyesha Watanzania kuwa timu hiyo inayouwezo wa kufanya vizuri kwenye mashindano ya Kimataifa wakiwa ni wawakilishi wa nchi katika mashindano hayo.
 
Uhuru Seleman
Kiungo wa Azam FC anasema mechi za kimataifa zina utofauti na ligi kuu, zinaangaliwa na watu wengi hivyo umakini ni njia pekee itakayotupa matokeo mazuri.
  “ Tumejiandaa vizuri, tumecheza mechi nyingi za kirafiki na ligi tunafanya vizuri nawataka wachezaji wenzangu atakayepata nafasi aitumie vizuri, afanye vizuri kwa faida yake, klabu na nchi kwa ujumla kwa kuwa sisi ni wawakilishi nchi” anasema Uhuru.
  Azam FC imepata nafasi ya kuingia kombe la Shirikisho Afrika, baada ya kumaliza ligi ya msimu uliopita 2011/2012 kwa kuwa washindi wa pili, baada ya mechi ya kesho dhidi ya timu hiyo ya Al Nasri Juba, mechi ya marudiano itachezwa wiki mbili zijazo nchini Sudani Kusini.
 
God Bless Azam FC, God Bless Tanzania!!

No comments:

Post a Comment