Mechi
za marudiano za raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL)
zinachezwa wikiendi hii katika viwanja kumi tofauti wakati mechi ya
Flamingo ya Arusha na Machava FC ya Kilimanjaro yenyewe itachezwa
Jumatatu (Mei 20 mwaka huu).
Uamuzi
wa mechi hiyo kuchezwa Jumatatu ni kutokana na Uwanja wa Sheikh Kaluta
Amri Abeid kutumika kwa mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kesho wakati
Jumapili utatumika kwa shughuli nyingine za kijamii kwa mujibu wa
wamiliki wa uwanja huo (CCM Mkoa wa Arusha).
Mechi
nyingine zitachezwa keshokutwa (Jumapili) ambapo Abajalo watakuwa
wenyeji wa Red Coast kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam. Uwanja wa Nangwanda Sijaona mjini Mtwara utatumika kwa mechi
kati ya wenyeji Coast United na Kariakoo ya Lindi.
African
Sports ya Tanga itaoneshana kazi na Techfort ya Ifakara mkoani Morogoro
katika mchezo utakaochezwa Uwanja wa Mkwakwani. Nayo Simiyu United ya
Simiyu itakuwa mgeni wa Magic Pressure ya Singida kwenye Uwanja wa
Namfua, mjini Singida.
Uwanja
wa CCM Kirumba jijini Mwanza ndiyo utakaotumika kuzikutanisha timu za
Polisi Jamii Bunda kutoka Mara na wenyeji UDC wakati Biharamulo FC ya
Kagera na Polisi SC ya Geita zitaumana kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini
Bukoba.
Milambo
FC ya Tabora itakuwa mwenyeji wa Saigon FC ya Kigoma kwenye Uwanja wa
Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora huku Mbinga United ya Ruvuma
ikiikaribisha Njombe Mji ya Njombe kwenye Uwanja wa Majimaji mjini
Songea.
Uwanja
wa Kumbukumbu ya Samora mjini Iringa utatumika kwa mechi kati ya
wenyeji 841 KJ dhidi ya Kimondo SC kutoka Mbeya. Nazo Rukwa United na
Katavi Warriors zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Nelson Mandela mjini
Sumbawanga.
Timu
zitakazofuzu kucheza raundi ya pili zitacheza mechi zao za kwanza kati
ya Mei 25 na 26 mwaka huu wakati mechi za marudiano ni kati ya Juni 1 na
2 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment