Kocha wa Bayern Pep Guardiola atakabiliwa na mtihani mwingine dhidi ya
timu ya premier League, katika Champions League baada ya kupata ushindi
wa kombe la Super Cup dhidi ya Chelsea kupitia mikwaju ya penalti.
Mlinda lango wa Bayern Manuel Neuer anasema huu utakuwa mchuano wa timu
mbili zenye nguvu sawa, wakati naye nahodha wa Manchester City Vincent
Kompany akiwataka wenzake wakaze buti baada ya kichapo cha mabao matatu
kwa mawili dhidi ya Aston Villa.
Katika kundi F, Arsenal ambao maisha yao yanaonekana kuwa ya starehe
wakati huu wakiongoza Ligi Kuu ya England, watakuwa wenyeji wa Napoli. Timu
zote mbili zilishinda mechi zao za kwanza za Champions League.
Kwa upande wao Borussia Dortmund wana shughuli pevu nyumbani dhidi ya Olympique
Marseille.
Baada ya kichapo cha nyumbani cha mabao mawili kwa moja na
West Bromwich Albion Jumamosi iliyopita katika Ligi ya nyumbani, mbinyo
unazidi kuongezeka dhidi ya kocha wa Manchester United David Moyes kabla
ya mpambano wao wa Jumatano ugenini na Shakhtar Donetsk katika kundi A.
Juventus watakuwa wenyeji wa Galatasaray katika mchuano wa kundi B
kati ya mabingwa wa Italia na Uturuki, ambao wamemkaribisha Roberto
Mancini kama kocha wao mpya. Real Madrid watakuwa nyumbani kupambana na
FC Copenhagen, kurejesha ujasiri wao baada ya kunyamazishwa mwishoni mwa
wiki katika mchuano wa ligi ya nyumbani waliofungwa bao moja kwa sifuri
na Atletico Madrid.
AC Milan inawakaribisha tena kikosini Riccardo Montolivo na Stephan El
Shaarawy baada ya kupona majeraha yao pamoja na Mario Balotelli ambaye
amepumzika vya kutosha, wakati watakapochuana na Ajax mjini Amsterdam
katika mechi ya kundi H hapo kesho.
Barcelona watasafiri mjini Glasgow kupambana na Celtic hapo kesho katika
mechi ya kundi H, bila ya huduma za mashambuliaji wao Lionel Messi.
Muargentina huyo alipata jeraha katika mguu wake wa kulia mwishoni mwa
wiki lakini Neymar yuko tayari kulijaza pengo hilo.
Atletico Madrid watasafiri hadi Porto katika mchuano wa kundi G. Real
Sociedad watajaribu kujikwamua ugenini dhidi ya Bayer Leverkusen katika
mechi ya kundi A. Schalke wa Ujerumani wako na kibarua dhidi ya Basel
katika mechi ya kundi E, baada ya timu hiyo ya Uswisi kubwaga Chelsea
mabao mawili kwa moja katika mchuano wa kwanza nao Schalke wakawapiku
Steaua Bucharest mabao matatu bila jawabu.
Sasa kocha wa Chelsea Jose
Mourinho anasema Juan Mata ataanza katika mchezo wa kesho dhidi ya
Steaua ambao ni lazima aishinde. Katika kundi C, Paris St Germain
watapambana na Benfica nao Anderlecht wakiwaalika Olympiakos siku ya
Jumatano.
No comments:
Post a Comment