Southampton ambao wameonyesha ukali watakumbana na kibarua chao
kigumu zaidi katika Ligi ya Premia msimu huu Jumamosi watakapokutana na
Arsenal ugenini.
Hata hivyo, hilo halimbabaishi hata kidogo meneja Mauricio
Pochettino, na wala haliwatishi mastraika wake matata Rickie Lambert na
Jay Rodriguez.
Saints au Watakatifu ukipenda wamo nambari tatu kwenye ligi baada ya
kucheza mechi 11, wakiwa na alama 22 ambazo ni tatu tu chini ya zile
walizo nazo Arsenal ambao wanaongoza ligi.
Lakini Pochettino anaamini kwamba Saints wanaweza kuwalima viongozi
hao wa ligi sawa na walivyowafanyia Liverpool walipokuwa wakiongoza ligi
mapema kwenye msimu.
"Ninafikiri itakuwa mechi sawa na ya Liverpool kwa sababu tulipokuwa
tukicheza nao walikuwa juu kwenye ligi,” raia huyo wa Argentina aliambia
televisheni ya Southampton ya Saints Player mnamo Alhamisi.
“Daima tumeamini kuwa tunaweza kushinda kila mechi tunayocheza.
Tunaamini kwamba tunaweza kucheza vyema sana kwenye mechi na tunaweza
kupata matokeo mazuri kutoka kwenye mechi hii – daima sisi huamini
hivyo,” akaongeza, akisisitiza imani ambayo imeiinua klabu hiyo kutoka pwani ya kusini katika
kiwango cha kadiri kwenye ligi kuu.
Pambano hilo linakuja baada ya muda wa mapumziko kwa ajili ya mechi
za kimataifa ambapo wachezaji watatu wa Saints waliitwa kuchezea
Uingereza kwenye mechi dhidi ya Chile na Ujerumani - Lambert, Rodriguez
na nahodha Adam Lallana.
Pochettino alisema Waingereza hao watatu wako vizuri kufanya vema ndani ya
klabu. “Nina furaha sana kutokana na uchezaji wao walipokuwa wakichezea
timu ya taifa,” alisema licha ya Uingereza kuchapwa mechi zote mbili.
“Nina uhakika kwamba uzoefu huo utawafaa sana kwa sasa na siku zijazo katika timu na pia labda katika timu ya taifa.
“Ni bayana kwamba msukumo na uzoefu waliopata wakichezea timu ya taifa vitatusaidia hapa Southampton pia."
Lambert, aliyengoza safu ya mashambulizi Saints waliposhindwa 6-1
uwanjani Emirates msimu uliopita, alisema anasubiri kwa hamu na ghamu
kurekebisha mambo.
“Nasubiri sana Jumamosi kwa sababu tunafanya vyema kwa sasa na ni
matumaini yetu kwamba tunaweza kupeleka uzuri huu kwenye mechi hiyo,”
Aliambia tovuti ya Southampton.
"Tutaenda huko tukiwa na imani. Tunajua itakuwa moja ya mechi ngumu
zaidi kwa sababu Arsenal wanacheza vyema kwa sasa.
Itakuwa ngumu, lakini
tuna imani kwamba tunaweza kwenda huko na kutoka na kitu.”
Rodriguez alieleza imani yake kwamba timu hiyo itafanya vyema msimu uliopita.
“Tutapelekea Arsenal mchezo na itakuwa mechi ngumu,” alisema.
“Mwaka uliopita ulikuwa jinamizi kwani tulichapwa 6-1 huko, lakini tuna
ujumbe tunataka kufikisha na tutafika huko tukikusudia hilo.”
No comments:
Post a Comment