Hayawi hayawi sasa yamekua!! Young Africans mabingwa
watetezi wa Ligi Kuu ya Vodacom leo wamekamata usukani wa kiti cha
uongozi baada ya kuichapa timu ya JKT Oljoro kwa mabao 3 - 0 katika
mchezo uliofanyika dimba la uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Baada ya mchezo wa leo wapenzi, washabiki na wanachama wa Young
Africans waliamsha shangwe uwanjani kufutia kupata matokeo ya timu za
Mbeya City na Azam ambao walikuwa wakiongonza Ligi kwa muda mrefu kutoka
sare ya mabao 3-3.
Kwa matokeo
hayo ya leo Young Africans imefikisha pointi 28 na mabao 31 ya kufunga
huku Azam ikifuatia kwa pointi 27 sawa na Mbeya City wakiwa na tofauti
ya mabao ya kufunga na kufungwa na Simba SC wakishika nafasi ya nne kwa
kuwa na pointi 24.
Ikicheza soka safi na la kuvutia Young
Africans ilianza mchezo kwa kasi kwa lengo la kusaka bao la mapema ili
kujiweka katika nafasi nzuri ya kuongoza Ligi na ndivyo ilivyokua kwa
vijana wa jangwani kupeleka furaha na shangwe kwa washabiki wake.
Saimon
Msuva aliipatia Young Africans bao la kwanza dakika ya 23 ya mchezo kwa
kichwa akiunganisha vizuri krosi ya kiungo mnyarandwa Haruna Niyonzima
aliyewatoka walinzi wa JKT Oljoro na kuukwamisha mpira wavuni.
Mara
baada ya bao JKT Oljoro waliendelea kujikanyaga wenyewe na al-manusra
Hamis Kiiza aipatie timu yake bao dakika ya 26 ya mchezo baada ya mpira
alioupiga kuokolewa na walinzi wa Oljoro na kuwa kona ambayo haikuzaa
matunda.
Dakika ya 30 Mrisho Ngassa aliipatia Young Africans bao
la pili kwa jitihada binafsi baada ya kuukokota mpira kuanzia kati kati
ya uwanja na kufumua shuti kali la umbali wa mita 25 na kutinga wavuni
moja kwa moja na kuongeza shangwe kwa washabiki wa Young Africans.
Mpaka ulikwenda mapumziko, Young Africans 2 - 0 JKT Oljoro.
Kipindi
cha pili cha mchezo kilianza kwa kocha mkuu Ernie Brandts kufanya
mabadiliko ambapo alimtoa Hamis Kiiza na nafasi yake kuchukuliwa na
Jerson Tegete ambaye aliongeza nguvu na uwezo wa kumiliki mpira.
Dakika
ya 54, Jerson Tegete aliipatia Young Africans bao la tatu na la ushindi
baada ya krosi iliyopigwa na Mrisho Ngassa kumkuta Tegete ambaye
aliukwamisha mpira wavuni na kuendeleza furaha kwa washabiki wake.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, Young Africans 3 - 0 JKT Oljoro.
Mara
baada ya mchezo wa leo, kocha Brandts ametoa mapumziko ya wiki kwa
wachezaji wake kufuatia wengi kujiunga na timu za Taifa na kikosi
kinatarajiwa kuanza mazoezi tena Novemba 24, 2013 kujiandaa na mzunguko
wa pili na mashindano ya kimataifa.
Young Africans: 1.Dida, 2.Twite, 3.Oscar, 4.Cannavaro 5.Yondani, 6.Chuji 7.Msuva 8.Domayo, 9.Kiiza/Tegete,10.Ngassa, 11.Niyonzima/Lusajo

No comments:
Post a Comment