CHACHA KUCHEZESHA MICHUANO YA AYG
Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limeteua
mwamuzi msaidizi wa Tanzania anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira
wa Miguu (FIFA), Ferdinand Chacha ameteuliwa kuchezesha michezo ya Vijana ya
Afrika (AYG- African Youth Games).
Michezo hiyo ya kwanza ya Afrika itachezesha jijini
Gaborone, Botswana kuanzia Mei 22-31 mwaka huu. Tanzania pia itashiriki katika
mashindano hayo ya vijana wenye umri chini ya miaka 15.
SIMBA, ASHANTI UTD KUVAANA TAIFA
Michuano ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) kuwania
ubingwa wa Tanzania Bara inaendelea kesho(Aprili 12 mwaka huu) katika raundi ya 25 ambapo Simba na Ashanti
United zitapambana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Mechi nyingine zitakuwa kati ya Tanzania Prisons na
Rhino Rangers (Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine, jijini Mbeya) wakati Coastal
Union itakuwa mwenyeji wa JKT Ruvu kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Keshokutwa (Aprili 13 mwaka huu) kutakuwa na mechi
nyingine nne za kukamilisha raundi hiyo. Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid
jijini Arusha utakuwa mwenyeji wa mechi kati ya wenyeji Oljoro JKT na Yanga.
Mtibwa Sugar itacheza na Ruvu Shooting (Uwanja wa
Manungu, Morogoro), Mgambo Shooting na Kagera Sugar zitaoneshana kazi kwenye
Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga huku Mbeya City ikiumana na Azam kwenye Uwanja
wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya.
TIMU YA WATOTO WA MITAANI YATAMBULISHWA BUNGENI
Timu ya Watoto
wa Mitaani ya Tanzania iliyotwaa ubingwa wa Dunia wa Watoto wa Mitaani nchini
Brazil baada ya kuifunga Burundi mabao 3-1 kwenye fainali imetambulishwa leo (Aprili
11 mwaka huu) katika Bunge Maalumu la Katiba mjini Dodoma.
Baadaye
timu hiyo leo itapata chakula cha mchana na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mizengo Pinda. Saa 10 jioni itatembeza kombe hilo katika maeneo
mbalimbali ya Manispaa ya Dodoma katika gari za wazi.
Jioni
imeandaliwa hafla maalumu ya chakula pamoja na burudani hapo hapo mjini Dodoma
ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk.
Fenella Mukangara.
BONIFACE WAMBURA
OFISA HABARI NA MAWASILIANO
SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA (TFF)
No comments:
Post a Comment