Bingwa wa ndondi wa ulimwengu katika uzani wa juu Vladmir Klitschko
ameamrishwa kulitetea taji lake la Shirikisho la Kimataifa la Ndondi –
IBF dhidi ya Kubrat Pulev wa Bulgaria ambaye hajawahi kushindwa pigano
lolote.
Pulev ana rekodi ya kucheza mapambano 20 akishinda yote huku mapambano 11 akishinda kwa KO.
Klitschko aliyatetea mataji yake ya WBA na WBO pamoja na mkanda wa IBF
wiki mbili zilizopita alipomwangusha sakafuni katika raundi ya tano
bondia Alex Leapai wa Australia.
Hilo lilikuwa pigano la lazima la kutetea taji lake la WBO, na sasa
Shirikisho la IBF limetangaza Pulev mwenye umri wa miaka 33 kama
mpinzano wao wa lazima.
Pulev ameukaribisha uamuzi huo akisema kwamba hiyo ni zawadi yake kubwa
ya kusherehekea siku yake ya kuzaliwa. Pulev anasema alishuhudia pigano
la Klitschko na Leapai na ni kweli kwamba Klitshcko hakuwa na kibarua
chochote dhidi ya mpinzani huyo.
Lakini anasema pigano lake na Mu Ukraine huyo litatimiza ndoto yake na
kuuonyesha ulimwengu kuwa Klitschko siyo mashine isiyoweza kushindwa.
Promota wa Pulev amesema tayari mazungumzo yameanza kuhusu pigano hilo
dhidi ya Klitschko.
No comments:
Post a Comment