Baada ya kushuhudia mechi ya kwanza ya fainali ya
kombe la dunia la mwaka huu huko Brazil,mamilioni ya mashabiki kutoka
bara Afrika hii leo watafungua macho na kupaza sauti zao wawakilishi wa
kwanza wa Afrika The Indomitable lions wa Cameroon ikitoana kijasho na
Mexico katika mechi ya pili ya kundi A.
Timu hizi zimewahi kukutana mara moja pekee
kabla ya hii leo.Mexico ilishinda mechi hiyo ya kujipima nguvu kwa bao
moja kwa nunge.
Mechi hiyo ilichezwa huko L.Angeles
Marekani mwaka wa 1993 ,lakini hii leo hii haitategemea historia wala
ukweli kuwa Mexico haijawahji kuishinda timu yeyote ya Afrika katika
kombe la dunia ,la dakika tisini katika uwanja wa Arena das Dunas,ulioko
Natal ndizo zitakazoamua yupi kati yao ni kidedea.
Kocha wa Mexico Miguel Herrera atakuwa bila ya
mshambulizi nyota Javier Hernandez kutokana na kuwa hajafunga bao lolote
katika mechi tisa.
Kocha huyo atawategemea Giovani dos Santos na
Oribe Peralta katika safu ya ushambulizi huku akitarajia Guillermo Ochoa
kulinda lango lake.
Kwa upande wao Cameroon ambao walifanya mgomo wa
marupurupu kabla ya kuabiri ndege ya Brazil ,nyota wao Samuel Etoo
anatarajiwa kuanza katika mechi hii licha ya kuwa hayuko timamu kiafya.
The indomitable Lions walifuzu kwa mashindano haya baada ya FIFA kubatilisha matokeo ya kichapo mikononi mwa Togo.
Kocha Volker Finke anakabiliwa na changamoto ya
mshikamano wa timu yake iliyowasili Brazil siku nne tu zilizopita baada
ya mgomo huo wa marupurupu.
Timu yake ndiyo yenye kushikilia rekodi ya kushindwa mara nyingi kuliko timu zote.
Cameroon imepoteza mechi 24 na kushinda mechi moja pekee kati ya 13 ilizoshiriki.
Cameroon iliilaza Saudi Arabia bao 1-0 mwaka wa 2002.
Katika mashindano haya Camerooon imemshirikisha
mchezaji mchanga zaidi katika kikosi chao Fabrice Olinga mwenye umri wa
miaka 18.
Uhispania vs Uholanzi
Mechi nyengine itakayokuwa ikitazamiwa na mamilioni ya mashabiki kote duniani ni Mabingwa watetezi wa kombe la dunia Uhispania .
Mabingwa hao huko Afrika Kusini mwaka wa 2010 wanafungua kampeini yao dhidi ya Uholanzi katika Arena Fonte Nova, Salvador.
Mechi hii itakuwa kumbukumbu ya fainali miaka
minne iliyopita lakini Kocha wa Uhispania Vicente del Bosque hana sababu
ya kuwa na wasiwasi kwani anajivunia kikosi dhabiti kinachosheheni
mabingwa wa dunia mabingwa wa kombe la Ulaya na mabingwa wa taji la bara
Uropa.
kati ya mechi kumi walizochuana Uhispania imeishinda Uholanzi mara tano na ikashindwa mara nne.
Kocha mpya wa Manchester United na Uholanzi
Louis van Gaal anamtegemea nyota wa united Robin van Persie Wesley
Sneijder na Dirk Kuyt kudhibiti tikitaka ya wahispania.
Bila shaka ukitaka kutizama janja na janjaure basi kaa kitako usubiri mechi hii.
Mechi ya mwisho hii leo itakuwa ya baina ya Chile na Australia.
Kinyume na mechi baina ya Uhispania na Uholanzi
itakayoshuhudia tiki taka mechi baina ya chile na Australia inatarajiwa
kuwa ya kasi na nguvu kutokana na mifumo ya timu hizo mbili.
Chile dhidi ya Australia
Australia haijawahi kushinda mechi yeyote ya
kombe la dunia wala alama yeyote ila ile waliojinyakulia mwaka wa 1974
walipotoka sare ya suluhu bin suluhu dhidi ya CHILE
'The Socceroos' wameshindwa na Chile katika mechi zao zote za kujipima nguvu.
Australia ambayo inaorodheshwa katika nafasi ya
62 katika orodha ya timu bora na shirikisho la soka duniani FIFA, ndiyo
timu ya chini kabisa katika orodha hiyo ya FIFA inayoshiriki katika
mashindano haya huko Brazil.
Kwa upande wao Chile wamewahi kushinda mechi mbili pekee kati ya 17 walizocheza za kombe la dunia.
Chile ilizilaza Honduras na Switzerland huko Afrika kusini mwaka wa 2010.
Wanamtegemea nyota wao Arturo Vidal kuwafungia mabao .
Australia kwa upande wao wanawategemea Mark Bresciano na Tim Cahill kusonga mbele katika hatua ya makundi
No comments:
Post a Comment