Fainali za kombe la dunia zimefunguliwa rasmi Alhamis(12.06.2014) nchini
Brazil, wakati wenyeji Brazil wakipambana na Croatia huko wenyeji
wakijaribu kuonesha hisia za tamasha la kanivale.
Polisi walifyatua mabomu ya kutoa machozi na risasi za mipira dhidi ya waandamanaji wanaopinga mashindano hayo mjini Sao Paulo.
Lakini mabingwa hao mara tano wa kombe la dunia Brazil waliwashangaza
mashabiki wao baada ya kufungwa goli ambalo limetokana na mchezaji wa
Brazil dakika 11 tu tangu kuanza mchezo huo wa ufunguzi katika uwanja wa
Corinthians mbele ya mashabiki 61,600 ikiwa ni pamoja na wakuu wa nchi
12.
Marcelo akaribia kuangua kilio
Mlinzi Marcelo alikaribia kutiririka machozi baada ya kuusindikiza mpira
katika wavu wake kutokana na krosi iliyopigwa na Ivic Olic wa Croatia.
Lakini mshambuliaji shujaa wa Brazil Neymar alisawazisha katika dakika
ya 29 ya mchezo huo. Brazil ikashinda kwa mabao 3-1.
Polisi wa Brazil walijenga ukuta mduara wa chuma kuzunguka uwanja huo
kuwazuwia waandamanaji kusogelea eneo hilo ambalo tamasha hilo kubwa la
kandanda litaendelea kwa muda wa wiki nne, ambapo Brazil imetumia kiasi
ya dola bilioni 11 kutayarisha.
Lakini waandamanaji waliokuwa na nia ya kuchafua sherehe hizo wakivalia
mashati meusi na kujifunika nyuso zao waliwasha moto kwa kutumia
takataka , kilometa chache kutoka katika uwanja huo baada ya polisi
wenye silaha kujaribu kutuliza ghasia katika saa kabla ya kuanza kwa
ufunguzi wa fainali hizo.
Maandamano yaendelea
Matayarisho ya kombe la dunia yamechafuliwa na miezi kadha ya
maandamano, yakiakisi hasira za umma kuhusiana na matumizi ya fedha za
maandalizi.
Lakini mji wa Sao Paulo na miji mingine kwa kiasi kikubwa ilikuwa tulivu
wakati mchezo ulipoanza. Bendera za rangi ya njano na kijani zilipepea
katika majengo mengi.
Lakini waandamanaji ambao walisababisha vurugu kubwa wakati wa kombe la
mabara , Confederations Cup, mwaka jana wameapa kuandamana katika uwanja
wa Sao Paulo.
Kocha Kovac akasirishwa na penalti
Kocha wa Croatia Niko Kovac ambaye alikuwa na hasira amesema mwamuzi
kutoka Japan aliyesimamia pambano hilo la jana alikuwa hayuko katika
kiwango chake, baada ya kutoa penalti kwa Brazil ambayo imebishaniwa na
kubadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo huo wa ufunguzi.
Croatia ambayo iko katika nafasi ya 18 ya orodha ya FIFA ya timu bora
duniani , ilikuwa ikijaribu kuzuwia na kuwatuliza Brazil katika kipindi
cha pili hadi pale refa Yuichi Nishimura alipoamua upigwe mkwaju wa
penalti baada ya mshambuliaji wa Brazil Fred kuanguka wakati akipambana
na mlinzi wa Croatia Dejean Lovren.
"Iwapo kuna mtu ameona kuwa ile ilikuwa penalti, anyooshe mkono. Siwezi kunyoosha mkono. Sikuona penalti, amesema kocha Kovac.
Kabla ya mchezo huo shabiki huyu aliifagilia Brazil na kusema:
"Brazil ina nafasi nzuri sana. Kikosi chake ni kizuri sana, upande wa mashambulizi na ulinzi pia."
Jioni ya leo(13.06.2014) Simba wa nyika , Cameroon , wataingia uwanjani
kupambana na Mexico katika mchezo mwingine wa kundi A, wakati mabingwa
watetezi Uhispania inaanza kampeni ya kurelijesha taji hilo mjini Madrid
kwa kupambana na Uholanzi katika mchezo wa kundi B.
No comments:
Post a Comment