TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
CHAMA cha
Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania
(TASWA), kimesikitishwa na taarifa za baadhi ya
waandishi wa habari za michezo kupewa vitisho wanapokuwa wanatekeleza
majukumu yao ya kazi.
TASWA imepokea
malalamiko kutoka kwa baadhi ya waandishi wa habari za michezo wakidai baadhi ya wanachama wa Yanga
a.k.a ‘Makomandoo’ wamewapa vitisho kabla
na baada ya mchezo kati ya Kagera Sugar na Yanga uliofanyika Jumatatu wiki hii Uwanja
wa Kaitaba Bukoba.
Sekreterieti ya
TASWA ilifanya mawasiliano ya haraka na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Onesmo
Kapinga ambaye alikuwa mkoani Kagera na amethibitisha pasi na chembe ya shaka
kwamba vitisho hivyo vimewanyima fursa ya kutekeleza majukumy yao ya kazi.
Tukio hili
limetuhuzunisha sana kwa sababu licha ya kuwajengea hofu baadhi ya waandishi wa
habari kushindwa kutekeleza majukumu yao ya kazi kikamilifu, lakini linaweza
kujenga chuki zisizo na msingi kati ya klabu hiyo na TASWA.
Wanachama na
mashabiki wa klabu kubwa hapa nchini Simba na Yanga wakubali changamoto za
viwanjani na wasitake kutafuta mahali pa kupeleka lawama zao pale wanapoona
matokeo mabaya kwa klabu zao.
Si nia ya TASWA
kutetea udhaifu kama upo kwa baadhi ya waandishi wa habari, lakini tunaona kwa
malalamiko yanayotolewa na baadhi ya makomandoo hao kwa wanahabari si mazuri na
hoja zao hazina mashiko ni kutapatapa.
Tunauomba uongozi
wa Yanga uwakemee mashabiki wake waachane na mambo yasiyo na msingi ambayo
hayana manufaa kwa klabu hiyo na ulimwengu wa soka hapa nchini. TASWA inataka
wanahabari wawe huru kutekeleza majukumu yao na hilo tuna hakika litafanyika.
Kamati ya Utendaji
ya TASWA inatarajiwa kukutana mwishoni mwa wiki ijayo kujadili suala hili la
vitisho kwa wanahabari na pia itajadili masuala mbalimbali ikiwemo kutaja mkoa
utakakofanyika Mkutano Mkuu wa mwaka wa chama.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
11/10/2012
No comments:
Post a Comment