Zambia,
wakiwa ugenini Kampala, wamefanikiwa kuwafunga wenyeji wao Uganda magoli
9-8 kupitia mikwaju ya penalti, na kujiweka katika nafasi nzuri ya
kuutetea ubingwa wao, katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwaka
2013, kufanyika nchini Afrika Kusini, mwezi Januari.
Mikwaju 20 ya penalti ilihitajika kubainisha ni
nani mshindi na aliyeshindwa, kufuatia Uganda kutangulia bao 1-0 katika
mechi ya mjini Kampala.
Patrick
Ochan alikosa penati yake na hivyo kuwanyima nafasi Waganda kusonga mbele huku wachezaji wa Uganda walikosa kuitumia nafasi yao vizuri ya
kuongoza katika mchezo, na hata pia katika mikwaju hiyo ya penalti,
kufuatia Zambia kushindwa kutumbukiza wavuni mkwaju wa mapema wa
penalti.
Uganda walikuwa wamejiweka katika nafasi nzuri,
hasa baada ya kukumbuka kwamba mjini Ndola walishindwa bao 1-0, na
katika mchezo wa Jumamosi, Geoffrey Massa aliwawezesha The Cranes kuongoza kwa kufunga bao katika dakika ya 27.
Lakini licha ya juhudi kubwa za kusaka bao la pili katika
muda wa dakika 90 halikuwezekana kwa Uganda, wakiongozwa na kocha
kutoka Uskochi, Bobby Williamason, na kushangiliwa mno na mashabiki wengi
wa nyumbani.
Kipa wa Zambia Kennedy Mweene alionyesha uhodari wake na kuiokoa Chipolopolo kutokana na mipira mingi ya hatari iliyo elekezwa langoni mwake.
Mara tu baada ya dakika 90 kumalizika na mchezo
kuingia katika mikwaju ya penalti, nahodha Chris Katongo, na ambaye
aliiwezesha timu yake kuwa mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika,
alishindwa kupata bao, baada ya kipa wa Uganda, Denis Onyango, kuzuia
mkwaju huo kutoka kwa nahodha wa Zambia.
Zambia iliibuka mshindi wa mashindano ya mwaka
huu ya Kombe la Mataifa ya Afrika, baada ya kuishinda Ivory Coast
kupitia mikwaju ya penalti, katika fainali ya Libreville, nchini Gabon.
Uganda ilikuwa nusra ishiriki katika fainali
zilizopita, lakini walishindwa kupata ushindi katika mechi yao ya mwisho
ya kufuzu, licha ya kwamba walikuwa uwanja wa nyumbani.
Mara ya mwisho kwa Uganda kushiriki katika mashindano hayo ilikuwa ni mwaka 1978, walipomaliza katika nafasi ya pili.
Katika matokeo mengine ya Jumamosi, Ghana na
Mali, na ambayo ni mataifa mawili yaliyofika nusu fainali katika
mashindano yaliyopita, yalijihakikishia nafasi ya kufika Afrika Kusini
mwaka ujao.
No comments:
Post a Comment