KWA MAWASILIANO ZAIDI TUMIA BARUA PEPE rockersports212@yahoo.com AU TUPIGIE KUPITIA NAMBARI 0767166607 AU 0717166607. KARIBU SANA. 66666666607 AU 0717166607

Wednesday, November 28, 2012

KAMATI YA ULINZI NA USALAMA MUHEZA KUFANYA MSAKO WA NYUMBA KWA NYUMBA KUTAFUTA MALI ZA MAREHEMU SHARO. MAMIA WAJOTOKEZA KUMZIKA WENGINE WAPOTEZA FAHAMU.

Serikali wilayani Muheza imeeleza kusikitishwa kwake na kitendo cha wizi kilichofanywa na baadhi ya watu wasiowaaminifu kwa kumuibia marehemu kila kitu alichokuwanacho wakati mauti yakimkuta.
Akitoa tamko kwa niaba ya serikali, Mkuu wa wilaya ya Muheza Subira Mgalu alisema kutokana na kitendo hicho yeye kwa kushirikiana na Kamati yake ya ulinzi na usalama ya wilaya hiyo itafanya msako wa nyumba hadi nyumba ili kupata mali za marehemu zilizoibwa.
“Napenda kuhakikishia umati huu uliokusanyika hapa hata sisi tumesikitishwa na kitendo hicho na tunaahidi kufanya msako wa nyumba hadi nyumba ili kupata mali za marehemu zilizoibwa na wahusika kufikishwa kwenye vyombo vya sheria”,alisema Mgalu.
Alisema wanaamini msako huo utakuwa ni fundisho kwa watu wengine wasiowaaminifu hasa pale ambapo wanategemewa kutoa msaada badala ya kujali maslahi zao binafsi hatua ambayo inatokana na baadhi ya wananchi kukosa uzalendo.
WAKATI HUOHUO 

Maelfu ya waombolezaji walijitokeza hii leo kushiriki mazishi ya msanii muigizaji na mwimbaji Hussein Ramadahni Mkiety (Sharomilionea) yaliyofanyika kijiji cha Lusanga Wilayani hapa huku baadhi yao wakipoteza fahamu.

Mazishi hayo yaliyoongozwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha mapinduzi (CCM) Nape Nnauye aliyemwakilisha Rais Jakaya Kikwete yalifanyika saa saba mchana katika makaburi yaliyopo nyumbani kwa mama wa msanii huyo kitongoji cha Jibandeni.

Waombolezaji hao walianza kumiminika kijijini Lusanga tangu jana
 jioni ambapo kamati ya mazishi iliyokuwa chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya ya Muheza, Subira Mgalu ambapo hii leo asubuhi ilianza kupokea idadi kubwa zaidi ya wageni kuanzia asubuhi.

Sala ya mazishi hayo iliongozwa na Sheikh Twaha Juma ambapo baada ya jeneza kutolewa ndani ya nyumba ya mama wa msanii huyo liliwekwa uwanjani na kuswaliwa na waumini kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Baada ya swala hiyo Sheikh Twaha aliamuru jeneza hilo kupelekwa kaburini ambapo waombolezaji walilibeba kwa kupokeza, waombolezaji hao walikuwa wamepanga mstari kutoka nyumbani hadi makaburini ukoo wa Mkiety yaliyoko umbali wa mita 100 kutoka nyumbani.

SALAMU ZA RAIS  KIKWETE .

Rais Jakaya Kikwete aliwakilishwa na Nape Nnauye katika mazishi hayo ambapo katika salamu zilizotolewa kwa niaba yake alisema Serikali imeguswa na msiba huo na kwamba iko pamoja na wasanii katika kuomboleza kifo cha Sharomilionea.

Alisema Serikali inathamini kwa kiasi kikubwa mchango wa wasanii wa tasnia ya filamu kwa jamii nchini na kwamba iko nao katika kuwaendeleza.

“Rais amenituma nimwakilishe katika msiba huu,anasema binafsi ameguswa sana na msina huu wa Sharomilionea kwa ni msanii ambaye alikuwa mbunifu na alikuwa akichipukia kwa hali ya juu katika fani ya uigizaji”alisema Nnauye.

Rais Kikwete kupiti kwa Nnauye alisema umefika wakati sasa kwa wasanii hao kuungana na kuhakikisha jasho lao halipotei wala kunyonywa na wajanja wengine wa kati ambao kila siku wamekuwa wakinufaika huku wasanii wakiendelea kurudi nyumba .

Nnauye alisema mbali ya wasanii wa filamu pia wasanii wa fani nyingine nao wanastahili kuungana kuhakikisha jasho lao linawanufaisha na siyo mtu mwingine ili kujiletea maendeleo wao binafsi na familia zao kwa ujumla .

Nauye alimkabidhi bahasha ya rambirambi ya msiba huo Rais wa
Shirikisho la filamu Tanzania (TAFF) Simon Mwakifwamba filamu ambapo hata hivyo hakuweza kutaja ni kiasi gani cha fedha kilichotolewa .

MAMA SALMA KIKWETE AWAKILSIHWA.

Katika msiba huo Mke wa Rais Jakaya Kikwete alituma salama za rambirambi zilizosomwa na Mkuu wa Wilaya ya Muheza Subira Mgalu ambapo alisema ameguswa na msiba huo na kuwataka ndugu wa Sharomilinoea pamoja na wasanii kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki cha msiba.

Kwa mujibu wa Mgalu ni kwa Mama Salma alituma salamu hizo za ramburambi akiwa kama Mwenyekiti wa mfuko wa wanawake na Maendeleo
(WAMA).

Alisema Mama Salma amesikitishwa na kifo cha Sharomilionea kwa sababu amekufa akiwa bado kijana mdogo ambaye familia yake ilitegemea kwamba angeweza kuwa msaada kwako.

“Mke wa Rais kama mnavyojua ni mama wa watanzania wote na ni mama wa wasanii hivyo msibba huu wa Sharomilionea umemgusa sana na ameitaka familia yake kuwa na moyo wa subira katika kipindi hiki cha
majonzi”alisema Mgalu.

 
WASANII WAANGUKA NA KUPOTEZA FAHAMU
Wakati maiti ikitolewa na kupelekwa makaburini baadhi ya wasanii waliofika kushuhudia maziko ya msanii mwenzao sharomilionea walianguka na kupoteza fahamu.
Mwandishi wa habari hizi ameshuhudia takriban wasanii 20 wakianguka huku baadhi wakibebwa na kutafutiwa maeneo ya wazi ili waweze kupata hewa na wengine walilazimika kupepewa hadi fahamu zilipowarudia.
Hata hivyo wale walioshindwa kabisa kurudi katika hali zao za kawaida walilazimika kufikishwa katika Hospitali ya wilaya ya Muheza Teule ili kupata huduma za matibabu.

No comments:

Post a Comment