Mlinzi wa
zamani wa kimataifa wa Tanzania ambaye kwasasa ana makataba na klabu ya Simba
Victor Nampoka Kosta amelishangaa benchi la ufundi la klabu yake kwa kuendelea
kumsugulisha benchi la timu hiyo.
Kosta pia
ameshangazwa na usajili usiokwisha wa wachezaji wengine walinzi wa kati ambapo
klabu hiyo imekuwa haishi kuchukua na kuwaancha wachezaji kibao katika eneo la
ulinzi wa kati na yeye akiendelea kuonekana kama si lolote si chochote.
Kosta ambaye kabla ya kurejea kwa mabingwa hao
wa soka wa Tanzania Bara ambao sasa ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya
vilabu bingwa barani Afrika akitokea nchini Mozambique katika klabu ya
Hidroelectrica de Cahora de Songo(HCB Songo), amesema yeye anajiamini kuwa bado
anawezea kutoa mchango wake kwa kiwango cha juu ispokuwa ni suala la kuaminiwa
na benchi la ufundi la timu yake.
Amesema
anajuta kurejea nyumbani kucheza soka katika klabu hiyo ambayo wakati akiwa HCB
Songo ya Mozambique uongozi wa Simba ulikuwa unamsumbua kwa kumpigia simu
arejee kuichezea klabu hiyo jambo ambalo sasa linamgharimu kwa kuwa HCB Songo
mpaka sasa bado inamhitaji.
Kosta
amesema amechoshwa na benchi la Simba ambalo linazidi kumfanya aonekane kama
mchezaji mstaafu wakati umri wake unamruhusu na uwezo wake bado ni mkubwa
kuliko walinzi wa kati wengi wakiwemo walinzi wa kati wanaochezea timu ya
taifa.
Ametolea
mfano mchezaji kama Nadir Haroub ‘Kanavaro’, Aggrey Moris na Shomari Kapombe
bila kutafuna maneno Victor Kosta ‘nyumba’ amesema wana uwezo wa kawaida sana
lakini kwakuwa wana aminiwa na makocha na kupewa nafasi ndio maana wanaonekana
wazuri ukilinganisha na wengine.
Amesema
ameondoka Mozambique huku viongozi wa klabu yake ya HCB Songo wakisikitika na
walikubali kwa shingo upande kwakuwa walimuamini sana katika ulinzi wa kati wa
timu yao ilikuwa ikifanya vizuri katika ligi nchini humo, lakini mapenzi yake
kwa Simba yalimfanya arejee nchini.
Ameishangaa
kamati ya usajili ya Simba kwa kuendelea kufanya makosa ya kufanya usajili wa
gharama kubwa kwa wachezaji wa kigeni wakati uwezo wao unafanana na wachezaji
wa nyumbani ambao wana mapenzi na uchungu na vilabu vyao wanavyochezea.
Amesema
mpira wa Mozambique uko juu ukilinganisha na Tanzania na kwenye ubora wa
viwango wametuzidi hivyo haoni sababu ya kuhangaika wakati wao waliotoka nje
walikuwa wanawaburuza wazawa wa nchi hizo ambazo ziko juu kisoka kuliko hapa.
Kosta
amemtaja Obadia Mungusa kuwa ni mlinzi wa kati mzuri ambaye alikuwa akiichezea
timu ngumu ya Mtibwa kabla ya kuhamia Simba ambako mpaka sasa anasugua benchi
na uwezo wake kuiendelea kushuka.
Hata hivyo
Victor Kosta alipoulizwa kama yuko tayari kupelekwa katika klabu nyingine kwa
mkopo amesema hayukoa tayari kwa hilo na kwamba anasubiri mkataba wake na Simba
umalizike ili akatafute maisha mengine ya soka sehemu nyingine.
“kaka siko
tayari kwenda kokote kwa mkopo, nasubiri mkataba wangu na Simba umalizike
nitafute mwelekeo, nashukuru nafanya mazoezi na wananilipa mshahara wangu”
“naipenda
sana Simba, Kinacho nisikitisha hakuna mtu mwenye uamuzi wa mwisho, mara kocha,
mara viongozi na mara mashabiki, kwa hiyo timu inayumba na wachezaji wanakufa
moyo, lakini napenda sana kuitumikia Simba ndio maana nilikubali kurudi
nchini”.
No comments:
Post a Comment