Kiungo wa
timu ya taifa ya Uganda ‘The Cranes’ Hassan Waswa yuko mjini Khartoum, Sudan kwa
majaribio na moja ya klabu kubwa ya nchini humo na Afrika mashariki na kati ya El Merriekh ambayo mara baada ya
kumalizika kwa michuano ya Tusker ya chalenji , klabu hiyo imekuwa gumzo kwa kuwataka kwa uhamisho
wa gharama kubwa wachezaji waliong'ara na kuahidi mishahara minono.
Kama
ilivyokuwa kwa El Merreikh FC Simba na Azam za Tanzania Bara nazo zilifuata
nyayo za Merreikh kwa kufanya mawindo ya chini kwa chini kutaka wachezaji wakubwa wa
ndani ya ukanda wa Afrika mashariki na kati huku kila moja ikiambulia angalau
mchezaji mmoja mmoja wa kuongeza nguvu kwenye mapungufu katika vikosi vyao.
Kwa wachezaji
wenye uwelewa mkubwa na wenye ufahamu wa kutosha juu ya nini wanafanya na nini
mikakati yao ya maisha na malengo yao ni yapi, hicho kilikuwa kipindi kizuri
cha kufanya kweli kwa kuweka dhamira moyoni na kujituma uwanjani ili kuwatamanisha matajiri
na viongozi wa vilabu vikubwa si tu ndani ya ukanda huu bali hata nje, kwani
michuano hiyo ilikuwa ilikonyeshwa moja kwa moja na kituo cha television cha Superspot.
Timu ya
wataalamu wa kusaka wachezaji ya klabu ya El Merreikh ilikuwa imeweka kambi
katika jiji la Kampala na kuendeleza mawindo yao ya wachezaji kwa makini sana ikihaha huku na huko kusaka taarifa za baadhi
ya wachezaji waliowavutia katika michuano ya chalenji ya cecafa ya mwaka huu
2012 ambayo Uganda ilitwaa taji hilo kwa mara ya 13.
Hassan Wasswa aliyeng’ara
vema katika sehemu ya kiungo ya timu ya taifa ya Uganda ni mmoja wa wachezaji waliofanya vema na sasa amesafiri kuelekea Khartoum akiwa na
mchezaji mwingine wa ‘The Cranes’ Mike Mutyaba aliyekuwa akichezea klabu ya
Vibers kuichezea El Merreikh.
Wasswa alikuwa ni mchezaji huru baada ya
mkataba wake na klabu moja ya nchini Uturuki inayocheza ligi kuu ya Kayseri
Erciyesspor kumalizika mapema mwaka huu.
Mwenyewe Wasswa
kabla ya kuanza kwa michuano ya Chalenji aliweka dhamira ya kujituma na
kujiweka sokoni kupitia michuano ya Chalenji ili kupata mkataba mpya wenye
donge nono. Na kweli ndoto zake zimetimia na sasa yuko Khartoum katika klabu
hiyo.
“nakwenda
kujituma katika timu ya taifa na kutumia uwezo wangu wote ili nipate mkataba na
nina hakika nitapata mkataba” amekaririwa Waswaa akisema kabla ya michuano ya
Chalenji.
Mchezaji mwenye
mipango sahihi na malengo chanya kwa mustakabali wa maisha yake ya leo na ya
baadaye, anatakiwa kuwa kama Hassan Waswaa nahodha aliyekiongoza kwa mafanikio
kikosi cha timu ya taifa ya Uganda mpaka kutwaa taji la 13 mwaka 2012.
Hebu fikiria
safari ya kutoka Uturuki akarudi nyumbani Uganda akiwa na dhamira sahihi, na baada ya michuano ya
Chalenji anapata klabu nyingine sasa nje ya Uganda na sasa yuko huko Sudan, hivyo ndiyo inavyotakiwa katika maisha ya kuhangaika katika uchezaji wa mpira.
Licha ya
Tanzania kupitia timu zake zote mbili za Kilimanjaro stars na Zanzibar Heroes
kupeleka wachezaji zaidi ya 50 nchini Uganda kushiriki michuano hiyo iliyokuwa
ikiangaliwa na watu wengi duniani, hakuna hata mchezaji mmoja aliyeonyesha
dhamira ya kutafuta mwelekeo mwingine nje ya klabu yake ya sasa mbali ya Mrisho
Ngasa kupewa ofa ambayo aliikataa kwasababu zake mwenyewe.
Kwangu mimi maamuzi ya Ngasa sitaki kuyaingilia kwa kuwa Ngasa ni mtu mzima mwenye mke wa mtoto, na anaitwa baba mwenye familia bila shaka anafahamu zuri na baya. Na katika hilo pengine nipingane na wengi wanao mfananisha Ngasa na mtoto mdogo ni wazi mnamdhalilisha kwa kuwa nilikuwa ni mmoja wa watu waliomsindikiza siku ya harusi yake kwa hiyo ni mtu mzima.
Pengine niwaweke sawa tu msije mkatumia tena lugha hiyo kumrudisha mtu utotoni wakati alishatoka huko kitambo, lugha nzuri pengine ingetumika ni Ngasa hana washauri wazuri na anahitaji msaada wa wakala wake au mtu mwenye uwelewa wa kutosha juu ya elimu ya ushauri ili amuongoze.
Pengine swali hapa ni nini alichozidi Wasswa, ni malengo ndani ya maisha yake. Wachezaji wa Tanzania wanafikiri zaidi soka la Simba na Yanga na ndio maana wengi wao baada ya kuvitumikia vilabu hivyo kwa mafanikio ndani ya muda mfupi wanapotea na wakihamia vilabu vingine mpira wote unakwisha hata kama umri wake ni mdogo na anastahili kuendelea kucheza soka kwa zaidi ya miaka mitano mbele.
Wachezaji wa Tanzania wanapaswa kupambana na changamoto mpya za kucheza na watu tofauti tofauti, iwe kwa kutafuta mwenyewe au kutafutwa na watu iwe ndani au nje ya nchi hilo litaukuza mpira wao na taifa kwa ujumla.
Wanapaswa kujifunza kwa akina Keita, Akufor,Okwi, Yaw Berko, Kipre Tcheche, Sunzu, Niyonzima, Kiiza na wengine ambao wamejiunga na vilabu vyetu kutoka nje wakitafuta maisha na sasa wanafanya vizuri katika timu zao za taifa kama Okwi na Kiiza.
Wasswa bila shaka ataimarisha uwezo wake akiwa na Merreikh ambao utaisaidia Uganda, na sisi na akiana nanihii wetu tunaendelea kumbwela mbwela daima dumu.
Mungu ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment