Rais wa shirikisho la soka nchini Leordigar Chilla Tenga. |
Rais wa shirikisho la soka
nchini Leodigar Chila Tenga jana alifanya mkutano na waandishi wa habari uwanja
wa taifa jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutolea ufafanuzi juu ya sakata la
mchakato wa uchaguzi mkuu wa shirikisho la soka nchini TFF nchini na ule wa
bodi ya ligi, kufuatia kuwepo na malalamiko ya baadhi ya wagombea kufuatia kuenguliwa
kwao katika kinyanyiro cha uchaguzi huo na kamati ya rufaa ya uchaguzi chini ya
mwenyekiti Iddi Mnginjola.
Maamuzi ya kamati hiyo yaliibua
maswali mengi kwa wagombea, jamii ya wapenda soka na wadau wa mchezo huo nchini,
huku baadhi ya wagombea tayari wakitinga mahakamani na wengine kuanza kufikiria
kuelekea mahakamani kupinga maamuzi hayo wakitishia kuelekea huko kuzuia
uchaguzi huo ulipangwa kufanyika hapo awali tarehe 24/02/2013 kabla ya kusitishwa na kamati ya uchaguzi hii leo.
Fukuto la pingamizi
lilianzia pale kamati ya uchaguzi inayoongozwa na mwenyekiti wake Deogratius Lyato alipowaengua wagombea kadhaa wa nafasi mbalimbali
kutokana na kile kilichoelezwa kuwa wagombea hao hawakukidhi sifa za kupewa uongozi
ndani ya TFF huku vigezo na sifa hizo zikianzishwa kuwa ni pamoja na wagombea
kukosa uadilifu na kutokuijua vizuri katiba ya TFF na wengine ni kutokana na kutokuwa
na upeo wa mambo ya uongozi wa mpira.
Sababu zilizo tolewa kwa kweli zilizua maswali mengi na kuanza kuleta mtafaruku mkubwa kiasi kiasi kufikiriwa kuwa kuna hali ya mizengwe imeigubika uchaguzi huo.
Deogratius Lyato |
Walioenguliwa mapema na
kamati ya uchaguzi chini ya Deogratius Lyato ni pamoja na Omari Mussa Nkwarulo
aliyeomba kuwania urais na Michael Richard Wambura aliyejitosa katika
kinyang’anyiro hicho akiomba nafasi ya Makamu wa Rais.
Wengine waliochujwa
wakiomba kugombea nafasi ya ujumbe wa Kamati ya Utendaji ni Abdallah Hussein
Musa, Mbasha Matutu, Charles Mugondo, Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja,
Eliud Peter Mvella, Farid Nahdi, Omari Isack Abdulkadir na Shafii Kajuna Dauda.
Kwa upande wa uchaguzi
wa Bodi ya Ligi Kuu aliyechujwa ni Christopher Peter Lunkombe aliyekuwa akiomba
nafasi ya ujumbe katika Kamati ya Uendeshaji.
Hata hivyo baadaye
kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF ilipokea rufaa mbalimbali kupinga uamuzi wa
Kamati ya Uchaguzi ya TFF kuhusiana na uchaguzi utakaofanyika Februari 22 na 24
mwaka huu.
Waliowasilisha rufani
mbele ya Kamati hiyo inayoongozwa na Iddi Mtiginjola ni pamoja na waombaji
uongozi saba walioenguliwa katika kinyang’anyiro hicho. Warufani hao ni Omari
Mussa Nkwarulo na Michael Richard Wambura walioomba kugombea urais na umakamu
wa rais.
Iddi Mtinginjola. |
Wengine ambao waliomba
ujumbe wa Kamati ya Utendaji kuwakilisha kanda mbalimbali ni Farid Nahdi
(Morogoro na Pwani), Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Omari Isack
Abdulkadir (Dar es Salaam), Eliud Peter Mvella (Iringa na Mbeya) na Shaffih
Kajuna Dauda (Dar es Salaam).
Warufani wengine ni
wadau ambao waliweka pingamizi dhidi ya baadhi ya waombaji uongozi katika TPL
Board na TFF, pingamizi ambazo zilitupwa mbele ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa
sababu za kiufundi.
Wadau hao waliokata
rufani ni Agape Fue dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Jamal
Malinzi kugombea urais, Medard Justinian dhidi ya Kamati ya Uchaguzi TFF
kupinga kumpitisha Athuman Nyamlani kugombea urais, na Frank Mchaki dhidi ya
Kamati ya Uchaguzi TFF kupinga kumpitisha Hamad Yahya kugombea uenyekiti wa TPL
Board.
Kamati ya rufaa ya
bwana mtinginjola iliketi kupitia rufaa hizo na kutoa maamuzi ambayo
yalionekana kuzidi kuichanganya jamii ya wapenda soka kiasi mpaka baadhi wadau
na viongozi wa nchi walionekana kuibuka na kuhoji kulikoni na kujaribu hata
kupinga maamuzi hayo ya kamati ya rufaa ya uchaguzi ambayo ni kamati huru ya
TFF.
Miongoni mwa vingozi
hao naibu waziri wa habari utamaduni na michezo Amos Makalla ambaye
alijitambulisha kama mdau ambaye alisikika kupitia redioni( Clouds fm na Redio
one stereo) akitoa kauli ambayo kwa namna moja ama nyingine ilizidi kuibua
hasira za wadau na kutoa mawazo yao kwa hisia kali kupinga maamuzi hayo kwa
kumuunga mkono.
Maamuzi ya kamati ya
Iddi Mtinginjola yalikuwa ni kama ifuatavyo;
Kanda ya Dar es Salaam
rufaa ya Shafii Dauda imeshinda na hivyo basi jina lake limerudishwa katika
kinyanyiro cha uchaguzi na kwamba maamuzi ya kamati ya uchaguzi
yametengeluliwa.
Kanda ya Dar es Salaam,
Omari Abdulkadiri rufaa ya yake imeshindwa na hivyo maamuzi ya kamati ya
uchaguzi yamebaki kama yalivyo.
Faridi Mbaraka Salim
Nahdi rufaa yake imeshindwa kwa kushindwa kutofautisha miaka yake ya kuzaliwa
kati 1966 na kuonekana amezaliwa 1972 .
Eliudi Peter Mvela
rufaa yake imeshindwa kwasababu ya kutokuwajibika kwenye kamati ya utendaji
akiwa mjumbe wa kamati ya utendaji alipashwa kutetea kile walicho kubaliana
ndani ya kamati ya utendaji lakini alikwenda kinyume na kile walichokubaliana
ndani ya kamati ya utendaji kwa mujibu wa ibara 36(3) ya katiba ya tff na ibara
ya 12(1)(b)(d).
Kanda ya Shinyanga
Mbasha Matutu rufaa yake imeshindwa kwa kuingilia mchakato wa uchaguzi
kushiriki kuandaa pingamizi dhidi ya mgombea mwenzake kwani imethibitika
alishiriki kutaka wenzake washindwe, hivyo alikosa uadilifu kwa mujibu wa
kifungu namba 9(7) cha katiba ya TFF.
Mwenyekiti wa bodi
Ahmed Yahya aliwekewa pingamizi kuwa yeye si mwenyikiti halali wa Mtibwa Sports
klabu, kamati imeaangalia katiba ya Mtibwa imeonekana kuwa mwenyekiti aliaacha
madaraka yake na madaraka yake yakaenda kwa makamu mwenyekiti ambaye alikuwa na
mamlaka ya kuitisha mkutano ambao ndio ungemchagua mwenyekiti na kuendelea
mpaka mkutano mwingine.
Kwa mujibu wa katiba ya
Mtibwa makamu mwenyekiti alitakiwa kuitisha mkutano wa kumchagua lakini badala
yake alikwenda kwenye bodi na kumkasimu madaraka ya mwenyekiti jambo ambalo si
halali kwa mujibu wa katiba ya Mtibwa, hivyo kamati imebaini kuwa si mwenyekiti
wa halali wa Mtibwa.
Kwa upande wa rufaa ya
Michael Richard Wambura ambaye anawania nafasi ya makamu wa Rais imeshindwa
kwasababu hana sifa ya uadilifu.
Mtiginjola amesema amri
iliyotolewa na kamati ya rufaa ya jaji Mkwawa haijabadilishwa mpaka sasa na
kwamba maamuzi ya kamati ya jaji Mkwawa kwamba Wambura hana uadilifu yako
palepale.
Mtiginjola amesema
Wambura alitakiwa kudai haki yake kupitia mahakama ya michezo ya kimataifa
(CAS), kukata rufaa dhidi ya maamuzi ya kamati ya jaji Mkwawa.
Katika nafasi ya Rais,
mkata rufaa Omari Mussa Mkwaruro, rufaa yake imeshindwa kutokana na kuonekana
hana upeo wa kutosha juu ya mambo ya soka na kutokuijua katiba ya TFF.
Mkwarulo alishindwa
kujibu hata swali la mipango yake ya baadaye endapo atashinda kiti cha Rais wa
TFF, ambapo alitoa majibu ya kushangaza kwani alisema ataanzisha mashindano ya
soka ambayo yatakwenda mpaka Malawi na watu wenye mabasi ndio watakao peleka
wachezaji, jambo ambalo liliishangaza kamati yake, hivyo kamati imeona kuna
udhaifu mkubwa wa upeo wake katika masuala ya soka na katiba ya TFF.
Kwa upande wa rufaa
aliyokatiwa Jamali Emily Malinzi, ni mwamba Malinzi amekosa sifa ya uzoefu
katika uongozi wa kujishughulisha na mambo ya soka kwa kipindi mfululizo cha
miaka 5 kwa mujibu wa kifungu cha 9(3) , licha ya kwamba kuna ushahidi kuwa
alikuwa katibu wa Yanga kutoka 2003 mpaka 2006 mwenyekiti wake alikuwa Fransis
Kifukwe, lakini hajatimiza miaka 5.
Ushahidi mwingine ni
kuwa yeye kama mwenyekiti wa chama cha soka mkoa wa Kagera nafasi ambayo
aliipata mwaka jana bado hajatimiza miaka 5 na pia hakuna ushahidi mwingine
wowote ulionyesha kuwa amekuwa kiongozi wa michezo sehemu nyingine yoyote.
Pili katika suala la
uadilifu kuna taarifa kuwa Malinzi alipinga kuunga mkono maamuzi na maagizo ya
shirikisho la soka duniani FIFA ambayo yanawataka wanachama wake ikiwemo TFF
kufanya mabadiliko katika katiba zao kwa kuundwa kamati mbalimbali ndani kama
vile kamati ya rufaa ya uchaguzi, jambo ambalo lilikuwa ni maagizo ya FIFA,
Malinzi akiwa kiongozi wa soka wa mkoa wa Kagera ambao ni wanachama wa TFF
alipingana na mabadiloko hayo ambapo aliwaita waandishi wa habari kuelezea juu
ya pingamizi hilo.
Mgombea aliyeenguliwa na kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF Jamali Emily Malinzi. |
Kwa mujibu wa
Mtinginjola amesema kamati yake iliona kuwa hatua hiyo ya Malinzi endapo atapitishwa
na kuchaguliwa kuwa Rais atairejesha nyuma TFF katika kipindi ambacho FIFA
ilitaka kuifungia TFF kwa sababu za kukinzana na maamuzi yake jambo ambalo
Malinzi kama mgombea anakosa sifa chini ya ibara 9(3) cha katiba ya TFF.
Malinzi amekosa sifa
chini ya vifungu mbalimbali ikiwa ni pamoja vifungu vya uchaguzi 9(3) kifungu
namba 29, 39(3), 12(b)(d) na kwamba rufaa dhidi yake iliyokatwa na Agape
Fueyake imeshinda.
Rufaa dhidi ya Athumani
Nyamlani imeshindwa kutokana na mrufani kushindwa kutoa ushahidi na maelezo ya
kina juu ya kile alichokuwa anakipinga dhidi ya Athumani Jumanne Nyamlani.
Medard Justinian
alikata rufaa dhidi ya Nyamlani kwa madai ya kutokuwa muadilifu kwani Nyamlani
aliisababishia hasara TFF kwa kuisababisha mamlaka ya mapato Tanzania TRA
kuipiga faini TFF jambo ambalo Medard alishindwa kulithibitisha mbele ya kamati
ya rufaa ya uchaguzi ya TFF kwa kutoa hoja na vielelezo juu ya madai yake hayo.
Shauri la pili dhidi ya
Nyamlani ilikuwa ni mrufani kuona kwamba Nyamlani ni mtumishi wa serikali kama
hakimu hivyo haitakuwa sahihi kwa Nyamlani kuitumikia TFF wakati huohuo akiwa
pia ni mtumishi wa serikali kama hakimu akihoji ikiwa Nyamlani atahamishwa
kituo cha kazi na kupelekwa nje ya mkoa wa Dar es Salaam itakuwaje, jambo
ambalo limepigwa kumbo na kamati ya rufaa ya uchaguzi ya TFF, kwani kwasasa
bado Nyamlani ni makamu mwenyekiti wa TFF nafasi ambayo ameitumikia akiwa ni
hakimu na hakuna malalamiko yoyote yaliokuja kwamba ameshindwa kazi zake akiwa
hakimu na akiwa makamu wa mwenyekiti wa TFF, hivyo kamati ya rufaa ya TFF
imeitupilia mbali rufaa hiyo dhidi ya Athumani Jumanne Nyamlani.
Rufaa ambayo iliibua hoja
na hata hasira kwa wadau ilikuwa ni ya kumuondoa katika kinyang’anyiro Jamali
Malinzi, na sababu zilizo tolewa na kamati ya rufaa ya uchaguzi kutokueleweka vizuri
kwa mgombea mwenyewe na wadau kwani kwa kumuondoa Malinzi ni kwamba katika
nafasi ya Rais anabaki mgomea mmoja tu Athumani Nyamlani lakini mbaya zaidi ni
vipi Malinzi aondoke kwa kigezo cha kukosa uzoefu wakati walishawahi kuingoza
klabu kubwa nchini kama Yanga kuanzia 2012-2015 na pia kwasasa ni mwenyekiti wa
chama cha soka mkoa wa Kagera.
Sababu ya pili ya
kwamba Jamali Malinzi aliongoza kikao cha chama cha soka mkoa wa Kagera kwa
lengo la kupinga utaratibu wa kufanya mabadiliko ya katiba ya TFF kwa njia ya
waraka tofauti na katiba ya TFF inavyosema na kwamba Jamali Malinzi alikosa
uadilifu.
Akijibu maswali ya
waandhishi wa habari wakati wa mkutano wake wa jana Rais Tenga alikiri kuwa huko
nyumba wakati akiutambulisha waraka aliwahi kusema kuwa suala la waraka lilikuwa
ni demokrasia hivyo wajumbe wa mkutano mkuu walikuwa na hiari ya kukubali au
kukataa na kwamba hili lilikuwa ni suala la demokrasi.
Hoja ikaibuka iweje kamati ya rufaa ya uchaguzi ilimuengua Jamali kwa kigezo hicho wakati kumbe wajumbe walikuwa
wakitumia demokrasi juu ya kukubali au kukataa waraka huo.
Rais Tenga
alishindwa kujibu swali hilo na badala yake akasema yeye kama Rais na wadau kwa
ujumla hawana sababu ya kupinga justice
na kwamba kunatikiwa kuwepo na nguvu ya hoja na akasema mgombea anaweza
kupitia njia ya kuomba mapitio mapya ya maamuzi ya kamati ya rufaa ya uchaguzi(review)
au anaweza kwenda kwa wakubwa akimaanisha kwenda FIFA na CAS(mahakama ya
kimataifa ya michezo).
Tenga pia akasema
matumaini bado yapo licha ya kwamba hana uhakika kwakuwa kuna review na kuna
uwezekano wa kwenda FIFA na CAS na kwamba wao kama TFF wako tayari kutoa msaada
kwa mtu ambaye atataka msaada wa kudai haki kupitia vyombo hivyo na kwamba endapo
wataulizwa na FIFA wako tayari kuwaita kuwaonyesha nini kilicho amualiwa na kamati
na kuwaruhusu FIFA kufanya uchunguzi lakini pia wana nafasi ya kwenda CAS
(mhakama ya michezo ya dunia).
Jambo lingine ambalo
Rais Tenga alionekana kubabaisha majibu yake kwa waandishi wa habari ni juu ya
kutetea suala matumizi ya waraka kupitisha mabadiliko ya katiba wakati katiba
ya TFF ina zungumzia kuwa mabadiliko ya katiba yatakuwa yakifanywa na mkutano
mkuu (General Assmbley).
Majibu ya Rais Tenga
yalishindwa kuwaridhisha waandishi walio wengi kuwa katika karne ya 21 mkutano
mkuu unaweza kufanywa kwa njia kama hiyo au kwa kupitia njia ya simu(
tele-conference) kitu ambacho ni kipya na hakipo katika katiba ya TFF.
Pia Tenga alijitetea
kuwa utaratibu huo ulilazimika kutumika kutokana na matatizo ya kifedha na
kwamba hilo lilikuwa ni suala la muongozo wa FIFA na kwamba mabadiliko hayo yalipaswa
kufanyika kwa haraka.
Swali lingine lilikuwa
ni kuhusu sifa ya miaka mitano kwa mgombea wa nafasi ya uongozi kupitia bodi ya
ligi (TPL Board) kwani katika mchakato wa uchaguzi kuna baadhi ya wagombea
wamepitishwa kugombea nafasi ya uongozi katika bodi hiyo ilhali sifa hiyo
wakionekana hawana, ambapo Rais Tenga alishindwa pia kujibu swali hilo na badala
yake akajibu kwa ujumla pia swali hilo hapaswi kulijibu yeye kwa kuwa bado
nafasi iko kwenye review na kwamba
kama kuna mtu anaona ameonewa anaweza kujenga hoja juu ya hilo ili aweze kupata
haki yake.
Hoja nyingine ilikuwa
ni juu ya sifa ya wajumbe wa kamati mbalimbali ambao wamekuwa wakitoa maamuzi
ambayo katika hali ya kawaida majibu yake yako wazi, licha ya kwamba wajumbe wa
kamati za uchaguzi na kamati ya rufaa ya uchaguzi wajumbe wake ni wanasheria.
Hapo ndipo suala la mtu
aliye mkatia rufaa Jamali Emily Malinzi, Agape Fue lilipo ibuka na kuchukua
nafasi yake ambapo muuliza swali alihoji juu ya ni sifa zipi zinatumika
kuwateua wajumbe wa kamati ya uchaguzi na kamati ya rufaa ambao wengi ni
wanasheria.
Hoja ilikuwa kamati ya
uchaguzi ya Deogratius Lyato iliondoa pingamizi la Agape Fue katika kamati ya
uchaguzi kutokana na kwamba mwekaji wa pingamizi hilo hakuonekana wakati wa
kusikilizwa kwa pingamizi lake kabla ya Agape Fue kurejea tena katika kamati ya
rufaa ya uchaguzi ya Iddi Mtinginjola ambapo pia hakuonekana wakati wa
kusikilizwa shauri lake.
Kamati ya Mtinginjola
ilitangaza kuwa rufaa ya Agape Fue imeshinda na kumuondoa Jamali Malinzi katika
kinyanganyiro wakati mtu huyo hajaonekana wala hajulikani ni nani na yuko wapi na
ana jinsia gani, vipi rufaa hiyo ikapitishwa wakati yeye mkata rufaa haonekani
mbali ya kumtumia wakili wakati wa kusikilizwa shauri la Malinzi kinyume cha
sheria.
Rais Tenga alishindwa
kujibu swali hilo kwa mara nyingine tena ambapo aliendelea kulijibu kwa kutaka
wapingaji wa maamuzi ya kamati ya rufaa ya uchaguzi wajenge hoja na kudai haki
yao kupitia review, kwenda FIFA na CAS jambo ambalo kimsingi ni kwamba Rais
Tenga alishindwa kujibu kutoa majibu stahiki.
Swali ni je wakati
uchaguzi ukiwa umepangwa kufanyika tarehe 24/02/2013 muda wa kupitia upya
rufaa, kwenda FIFA na CAS unatoka wapi wakati ni siku saba tu zimesalia kabla
ya uchaguzi huo kufanyika.
Na je hotuba na majibu
ya Rais Tenga yalipaswa kuja wakati huu
ambapo uchaguzi uwewadia.
Pengine wengi
walitarajia Rais Tenga angekuja na majibu chanya zaidi ambayo yangeweza
kutuliza hali ya hewa tofauti na ilivyo sasa ambapo wengine wamesha kwenda
mahakamani na kinacho subiriwa ni amri ya mahakama(samance) ya kusimamisha
uchaguzi huo.
Mapema kabla ya mkutano
wa Tenga kukutana na waandishi wa habari, kulikuwa na kikao cha kamati ya
utendaji ya TFF kilichokuwa kikifanyika hapo hapo uwanja wa taifa ambacho
kilikuwa kinajadili juu ya mustakabali wa hali ya mchakato wa uchaguzi na mustakabali
wake.
Bila shaka hayo ndio
matokeo ya sehemu ya maamuzi yao ambayo Tenga alikuja kuwasilisha kwa wadau
kupitia kwa waandishi wa habari.
Labda niseme tu na haya
ni maoni yangu, kuwa Tenga ameunda kamati nyingi kwa umakini mkubwa sana na
kamati hizo zimeijengea heshima kubwa TFF, lakini kwa haya yanayotokea sasa si
Mntinginjola na Lyato pekee wanaodhalilika na kushushiwa heshima zao bali pia
hata Tenga mwenyewe kwa kuwa maamuzi mengi ya kamati hizi mbili hayakuzingatia
matakwa ya katiba na kanuni za uchaguzi za TFF.
Hatujui wakati Ashfrod
Mamelod akitarajiwa kuwasili nchini jumatatu kwa ajili ya kusimamia zoezi la
uchaguzi wa TFF, nini ataandika kuhusu uchaguzi huu ambao mwelekeo wake
kuvurugika kabisa na pengine kuingiliwa na serikali na kisha Tanzania kufungiwa
katika soka la kimataifa linalo simamiwa na FIFA.
Mungu tusaidie, Mungu ibariki
Afrika, Mungu ibariki Tanzania.
No comments:
Post a Comment