Kampuni ya Tanzania Mwandi kwa kutambua kuwa Tanzania na Afrika nzima kuna vijana wengi ambao wana vipaji vya mpira wa miguu na hivyo wanachohitaji ni kuonyeshwa tu jinsi ya kuufikia ‘Ulimwengu Halisi’ wa Mpira duniani Tanzania Mwandi imeamua kuanzisha michuano ya African Youth Football Tournament ambayo itawashirikisha vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 21.
Michuano hiyo
itaambatana na mafunzo kwa siku tano ambapo vijana hao watapata mafunzo ya
mpira wa Miguu (elimu, ujuzi na hata mbinu za uwanjani) kutoka kwa makocha
wawili wa hapa nchini na watatu wa kimataifa kutoka nje ya nchi, kuanzia tarehe
10/06/2013 hadi tarehe 14/06/2013 katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Aidha, mafunzo
yatafanyika nyakati za asubuhi na jioni wachezaji hao watashiriki Mashindano ya
kucheza wao kwa wao ili kupata vijana 11 bora miongoni mwa wachezaji
watakaoshiriki.
Wachezaji Bora 11
watakaopatikana watakuwa mabalozi wa Mdhamini Mkuu wa Michuano ya African Youth Football Tournament na watapata
fursa ya kutangazwa zaidi kimataifa na kutafutiwa vilabu vya kucheza soka
Barani Ulaya katika nchi nane (Ufaransa, Ureno, Uswis, Ubelgiji, Uholanzi,
Norway, Sweden na Denmark pamoja na barani Afrika na Asia.
Ili kupanua wigo wa
kuwatangaza kimataifa wachezaji wengi zaidi, Michuano hii pia itaalika skauti
na mawakala wa soka wa kimataifa ili kufuatilia uwezo wa wachezaji hao asubuhi
katika mazoezi na jioni kwenye michuano, kuwapata vijana bora ambao
watapendelea kuwatafutia timu nje ya nchi kukipiga huko kwa makubaliano ambayo
pande hizo mbili (mchezaji na wakala) zitaafikiana.
Miongoni mwa Mawakala
ambao watakuwepo ni wakala wa Kimataifa wa Tanzania, Dk. Damas Ndumbaro,
Phillip Mwakikosa (Sweden) na wengine wengi.
Hata hivyo kutokana na
gharama kubwa za uandaaji wa Michuano hii, na ndio kwanza ikiwa inaanzishwa,
Kampuni ya Tanzania Mwandi kwa kujali mahitaji ya Kitanzania tumeweka kiingilio
kwa mchezaji wa Tanzania kuwa shilingi laki tatu (Tsh. 300, 000) na mchezaji wa
nje ya Tanzania Dola 500 za Kimarekani (USD 500).
Fedha hizo zitagharamia
malazi, chakula na mahitaji mengine yote kwa mchezaji pindi atakapokuwa
kambini.
Hii ni fursa adimu kwa
vijana wa Kitanzania kuonyesha uwezo wao ili kutimiza ndoto za kucheza soka
barani Ulaya, Asia na barani Afrika katika vilabu vikubwa huku ikikumbukwa kuwa
mnamo Mwaka 2012 ni wachezaji wachache sana wa Kitanzania waliopata fursa ya
kufanya majaribio ya kucheza soka la kulipwa kutokana na uchache wa mawakala na
gharama hivyo kuletwa mawakala hao nyumbani Tanzania ni fursa pekee ya kufikia
malengo.
Mpaka sasa tayari
Kampuni ina majina takribani ya vijana 10 wa Nje ya nchi (Uganda, Nigeria na
Ghana) ambao wameomba kushiriki hivyo tunatoa wito kwa Watanzania kutoipoteza
fursa ya kuletewa njia ya kuelekea kusakata soka Barani Ulaya mlangoni mwao.
Lakini tunafahamu hali
halisi ya maisha yetu kwahiyo nitoe wito kwa Wadhamini mbalimbali ambao
tumewaomba kutusaidia kufanikisha Mashindano haya ambayo naamini yatalitangaza
taifa letu na kulitangaza zaidi soka letu kimataifa. Pia udhamini wao
utatuwezesha kupunguza hizi gharama kwa washiriki kutoka Tanzania na hivyo
kuwachukua vijana wengi zaidi.
Kampuni ya Tanzania
Mwandi ni Kampuni binafsi ambayo imejikita katika kuendeleza sekta za utalii,
michezo na burudani ndani na nje ya nchi na hivyo kuiongezea kipato nchi moja
kwa moja ama kupitia kuwawezesha wananchi kama vile kuwatengenezea fursa za
ajira vijana kupitia michezo.
No comments:
Post a Comment