Kazi ya ujenzi katika Uwanja utakaochezewa mechi za
kombe la dunia la soka mwaka 2014 nchini Brazil zimesimamishwa baada ya
jaji wa mahakama kusema kuna wasiwasi kuhusu usalama.
Uwanja huo wa Arena da Baixada katika jiji la
Curitiba ulipangiwa kuchezwa mechi nne za kombe la dunia. Ukarabati wa
uwanja huo ulikwishacheleweshwa kwa kipindi kadhaa.
Jaji Lorena Colnago alisema maisha
ya wafanyikazi yanahatarishwa kutokana na hali ya kuzorota kwa ujenzi
huo. Akiongeza kusema kuna hatari ya kuzikwa,kukanyagwa na magari na
hata kudondoka kutoka kuta za juu za uwanja huo.
Aliamrisha ukaguzi mpya ufanywe kabla ya kuanza
tena shughuli za ujenzi. Akiongeza kusema kumegunduliwa kasoro nyingi
katika ujenzi huo.
Taarifa hizo zinakuja wiki moja tu baada ya
uchunguzi kufichua kwamba wafanyikazi walioajiriwa katika ujenzi wa
mradi mwingine wa kombe la dunia walikabiliwa na hali ya kitumwa.
Wachunguzi hao walisema pia kwamba zaidi ya
wafanyikazi 100 walioajiriwa katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sao
Paulo wanaishi katika hali duni karibu na uwanja huo.
Mnamo mwezi wa Agosti, waziri wa michezo Aldo
Rebelo alisema ana wasiwasi jinsi ujenzi ulivyochelewa katika viwanja
vitano vya michuano ya kombe la dunia mwakani.
Baada ya ziara yake nchini Brazil, katibu mkuu
wa FIFA Jerome Valcke,alisema viwanja vyote lazima viwe tayari ifikapo
mwezi Desemba na kuonya hatavumilia tena kuchelewesha ujenzi na hakuna
'mpango mbadala'.
Michuano ya kombe la dunia imepangwa katika viwanja 12 nchini kote Brazil.
No comments:
Post a Comment