Shirikisho la Mpira
wa Miguu Tanzania (TFF) limepokea kwa masikitiko taarifa za ajali ya meli ya Mv
Skagit iliyotokea jana (Julai 18 mwaka huu) na kupoteza maisha ya karibu abiria
100 waliokuwemo kwenye chombo hicho.
Ajali hiyo mbaya
iliyotokea karibu na Kisiwa cha Chumbe, Zanzibar na kusababisha vifo vya watu
wengi ni msiba mkubwa, si kwa wadau wa mpira wa miguu pekee, bali kwa wananchi
wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Hivyo tunatoa pole na
salamu za rambirambi kwa ndugu wa marehemu, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar
(SMZ) na wote walioathirika na kuguswa na msiba huo mkubwa.
Kutokana na msiba huo, mechi mbili za leo kuwania Klabu
bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) kati ya Atletico ya Burundi
na El Salam Wau ya Sudan Kusini na ile ya Mafunzo ya Zanzibar dhidi ya Tusker
ya Kenya zitachezwa huku wachezaji wa timu zote wakivaa vitambaa vyeusi.
Mbali ya vitambaa
hivyo, pia kutakuwa na dakika moja ya kukaa kimya kwa ajili ya kuomboleza vifo
hivyo kabla ya kuanza mechi hizo zitakazochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mechi ya kwanza itaanza saa 8.00 mchana wakati ya pili itachezwa kuanzia saa
10.00 jioni.
No comments:
Post a Comment