Benki ya
CRDB PLC imeibuka mshindi wa tenda ya kutengeneza tiketi za elektroniki za
kuingilia uwanjani iliyotangazwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF).
Kampuni saba
zilijitokeza katika hatua ya awali ya kuonesha nia (Expression of Interest) kwa
ajili ya tenda hiyo ambapo Aprili 19 mwaka huu Kamati ya Mipango na Fedha ya
TFF ambayo ndiyo Bodi ya Tenda ya shirikisho ilipitia maombi hayo na kupitisha
nne kati ya hizo.
Baadaye
kampuni hizo nne; CRDB Bank PLC, Prime Time Promotions, Punchlines (T) Limited
na SKIDATA People Access Inc. zilitakiwa kuwasilisha rasmi tenda zao zikionesha
jinsi zitakavyofanya shughuli hiyo pamoja na gharama ya utengenezaji kwa tiketi
moja.
Bodi ya
Tenda ya TFF ilikutana Julai 13 mwaka huu kwa ajili ya kupitia tenda hizo
ambapo kampuni zote nne zilifanya uwasilishaji (presentation) wa jinsi
zitakavyofanya shughuli hiyo, na baadaye kuipa kazi hiyo benki ya CRDB.
Uamuzi huo
wa Bodi ya Tenda uliwasilishwa mbele ya Kamati ya Utendaji ya TFF. Kamati ya
Utendaji ya TFF katika kikao chake kilichofanyika Julai 14 mwaka huu iliridhia
uteuzi huo wa benki ya CRDB.
Baadhi ya
vigezo ambavyo Bodi ya Tenda ya TFF iliangalia na kuipa CRDB tenda ni uwezo wa
kufanya kazi hiyo (capacity), hadhi yake mbele ya jamii (credibility) katika
shughuli inazofanya na teknolojia ya kisasa itakayotumika kutengeneza tiketi
hizo.
Uamuzi wa
TFF kutangaza tenda hizo ulilenga kuimarisha udhibiti wa mapato ya milangoni na
kurahisisha mtiririko mzima wa washabiki kupata tiketi na kuingia viwanjani.
Rais wa TFF,
Leodegar Tenga amesema: “Hatua hii ni muhimu sana, kwani tulikuwa tukiisubiri
kwa muda mrefu. Si tu itaimarisha udhibiti wa mapato, bali pia itaondoa matatizo
ya tiketi na kuendelea kujenga credibility (kuaminika) ya TFF. Mafanikio haya
si kwa TFF pekee bali mpira wa miguu kwa ujumla.”
CRDB imeanza
mara moja mchakato wa shughuli hiyo ambapo tiketi hizo zinatarajia kuanza
kutumika rasmi katika kipindi cha kati ya miezi miwili na mitatu kuanzia sasa.
No comments:
Post a Comment