CHAMA cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania (TASWA)
kimeamua kulipeleka kwa Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT) kilicho chini ya mwenyekiti wake Dr Reginald Mengi,
suala la kuzuia televisheni na redio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi
Kuu Tanzania Bara pamoja na wapiga picha za televisheni kuchukua picha kwa
ajili ya kutumia kwenye habari.
Hatua hiyo ya TASWA ina lengo la kuomba mwongozo kwa chama hicho
ambacho ndio kinachomiliki vyombo vya habari kuhusiana na suala hili ambalo
limekuwa likilalamikiwa kwa kiasi kikubwa na wanachama wetu.
Tayari TASWA imefanya mazungumzo ya awali na MOAT, ambayo
imeridhia iandikiwe barua rasmi ili jambo hilo lijadiliwe kwenye vikao vyake na
baada ya hapo TASWA itapewa mwongozo ambao itautoa kwa waandishi wa habari za
michezo.
Kwa kuwa Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto pia ni mjumbe wa MOAT,
basi suala hilo tunaamini litafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo, hivyo
tunawaomba waandishi wa habari za michezo waendelee kuwa watulivu na wavumilivu
kipindi hiki na wafanye majukumu yao kama kawaida.
Siku zote chama chetu kimekuwa na uhusiano mzuri na Shirikisho
la Soka Tanzania (TFF) na wadau wengine wote na TASWA haitaki ifike mahali iwe
na mgogoro na chama chochote cha michezo, lakini pia haitakuwa tayari kuona
wanachama wake wakishindwa kutekeleza majukumu yao.
Kama mnavyojua wiki iliyopita kulifanyika kikao cha Kamati ya
Ligi na baadhi ya klabu zinazoshiriki ligi hiyo kuhusiana na tukio la kuzuia
televisheni na redio kutangaza moja kwa moja michezo ya Ligi Kuu pamoja na
wapiga picha za televisheni kuchukua picha kwa ajili ya kutumia kwenye habari.
Katika kikao hicho ambacho Mwenyekiti wa TASWA, Juma Pinto alihudhuria kulitoka maelezo mbalimbali ambayo
baadhi ya wanahabari hawakubaliani nayo na wamekuwa wakitaka TASWA ichukue
hatua uamuzi mgumu.
Sekreterieti ya TASWA imeona si vizuri kukurupuka kuchukua
uamuzi wowote ule kwa sasa kwani yenyewe haina chombo cha habari, lakini
wanaofanya kazi kwenye vyombo vya habari ndiyo wanachama wake. Itawasilisha
MOAT maazimio ya kikao cha Kamati ya Ligi kuhusiana na jambo hili, tuna hakika
tutalimaliza.
No comments:
Post a Comment