KWA MAWASILIANO ZAIDI TUMIA BARUA PEPE rockersports212@yahoo.com AU TUPIGIE KUPITIA NAMBARI 0767166607 AU 0717166607. KARIBU SANA. 66666666607 AU 0717166607

Wednesday, January 9, 2013

SUNDAY KAYUNI -MIAKA NENDA MIAKA RUDI WAAMUZI WATANZANIA HAWACHEZESHI AFCON NA KOMBE LA DUNIA KUNA TATIZO GANI KWENYE KITENGO CHAKO CHA UFUNDI. HIVI KWELI SYLVESTER KIRWA ANAMZIDI NINI ODEN MBAGA?

Mkurugenzi wa ufundi wa TFF Sunday Barton Kayuni. 
Shirikisho la soka duniani FIFA limetoa beji zake kwa waamuzi 13 wa Tanzania wakiwemo waamuzi watano wa kati ambao karibu wote ni wale waliokuwepo katika orodha ya waamuzi wa kati toka mwaka jana.
Akiwataja waamuzi hao kwa waandishi wa habari, afisa habari wa TFF Bonface Wambura amesema kuna upungufu wa maamuzi wawili kutoka katika orodha iliyopitishwa huko nyuma na FIFA, ambapo badala ya waamuzi 15 wa awali waliokuwa na beji hiyo sasa kuna waamuzi 13.
Waamuzi wakati ambao majina yao yamerudi tena yakiwa na beji hiyo ni pamoja na waamuzi 5 wa kati ambao ni Israel Mujuni, Oden Mbaga, Sheha Waziri, Judith Gamba(mwanamke) na Ramadhani Kibo.
Waamuzi wasaidizi ni Ally Kinduru, Ferdinand Chacha , Samweli Mpenzu, Hamisi Chang’walu, John Kanyenye, Mwanahija Makame(mwanamke), Josephati Burali, Erasmo Clemence.
Kwangu mimi idadi ya waamuzi wenye beji hiyo kupungua kwa waamuzi wawili tu wala hainipi homa, kinachonisumbua ni kuona waamuzi wa Tanzania wanaendelea kuwa ni waamuzi wa ligi za soka nchini Tanzania peke yake na si katika michuano mikubwa kama fainali za mataifa ya Afrika AFCON na kombe la dunia.
Nimezoea kusikia na kuambiwa na TFF kuwa waamuzi wa Tanzania wameteuliwa kwenda kuchezesha michezo ya klabu bingwa Afrika na kombe la shirikisho barani Afrika tena ile michezo ambayo wala haina mvuto, lakini inapofika michuano mikubwa kama AFCON unachoka kabisa kwani hakuna hata harufu ya majina ya watanzania katika uteuzi wa waaamuzi.
Vita yangu naielekeza ndani kabisa ya kitengo cha ufundi cha TFF kinachoongozwa na kaka yangu ninaye muheshimu sana katika tasnia ya soka Sunday Burton Kayun ambaye mbali ya kuwa mchezaji wa kiwango cha juu kabisa katika miaka ya nyuma pia ni kocha mkubwa na mwenye historia nzuri ya kufundisha mpira wa miguu.
Naanza kwa kumuuliza ndugu yangu tatizo nini? Mbona tunaendelea kukanyagwa wa CAF na FIFA na wewe upo? Basi hata kukoroma kidogo wajue kuwa upo ofisini na unatimiza wajibu unashindwa kuwakoromea hao CAF kwa tabia yao ya kutufanya hatujui kitu.
Naomba usinijibu kwa majibu rahisi na pengine ukatupia lawama kwa chama cha waamuzi FRAT na kamati yenu mliyounda ya waamuzi, hili ni la kwako bwana Kayuni. Hii ni aibu kukosa waamuzi kutoka Tanzania katika fainali za mataifa ya Afrika AFCON  na kombe la dunian kila mwaka yanapofanyika.
Swali lingine kwani wao wanatuzidi nini kama sheria 17 ni zilezile na tafsiri yake ni ile ile mabadiliko ni kidogo sana na yanategemea kama kuna haja ya kufanya hivyo.
Kaka kitengo kimekushinda hakuna faida ya semina wala kopa test za waamuzi za kila mwaka.
Wenzetu wamesikitishwa sana kwa taifa la soka kama Nigeria lenye sifa kubwa katika soka duniani na wakiendesha ligi ngumu ya soka nchini kwao kwa kuona shirikisho la soka barani Afrika CAF kwa mara nyingine likiendelea kuwapuuza waamuzi wa Nigeria mara baada ya kutangaza jumla ya waamuzi 18 ambao watasimamia michezo ya fainali za mataifa ya Afrika nchini Afrika kusini kuanzia January 19 mpaka February 10.
 Na Rockersports ikajaribu kuangalia kwa makini orodha hiyo kurudia na kurudia bila mafanikio ya kuona angalau safari hii pengine wamewanyima Nigeria labda tumepewa sisi na pengine tumekumbukwa kwa mwamuzi wa Tanzania japo mmoja kuchezesha michezo ya fainali hizo kubwa zenye heshima barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Katika orodha hiyo kuna mwamuzi wa pembeni wa siku nyingi kutoka nchini Nigeria Edibe Peter Elgam naye akiwemo katika orodha ya waamuzi wa pembeni 21 hapo ndipo nilipo mkumbuka Hamisi Changwalu, Samweli Mpenzu na John Kanyenye wa Tanzania ambao karibu kila mwaka wanarejeshwa katika orodha ya waamuzi waliopata beji ya FIFA lakini wanaishia kuchezesha Simba na Yanga, Mtibwa na Azam au JKT Ruvu na Mgambo JKT. 
Kuna waamuzi wawili kutoka nchini Afrika kusini ambao ni si wamuzi wazoefu sana Daniel Bennett na Zakhele Siwela ambao wanaendelea na kazi ya kutafsiri sheria 17 viwanjani na kumefanyika mabadiliko katika kundi la waamuzi wa kati wawili tu lakini katika kundi la waamuzi wa pembeni kuna waamuzi wapya 8 kutoka wale waliosimamia michezo ya fainali ya mwaka jana kule Equatorial Guinea na Gabon mwaka mmoja uliopita.
Hapo ndipo nilipo tazama tena katika mabadiliko ya waamuzi wasaidizi 8 hivi kweli waamuzi wa Tanzania wamekosa sifa ya kuchomekewa katika hao wapya 8 kuelekea nchini Afrika kusini kunako AFCON? Nilibaki nimeduwaa na nikitoa neno labla kuna namna au inawezekana tumerogwa. 
Orodha ya waamuzi wa AFCON 2013 imemjumuisha mwamuzi wa kati kutoka nchini Mali ambaye anaaminika kuwa mwamuzi bora kuliko wote barani Afrika na mwenye uzoefu wa muda mrefu huyu si mwingine bali ni Kolan Coulibaly.
Komlan Coulibaly alikuwepo kwenye fainali za mwaka 2010 nchini Angola kama ilivyokuwa kwa Badara Diatta ambaye baadaye alikabidhiwa filimbi katika mchezo wa fainali kati ya Zambia na tembo wa  Ivory Coast mjini Libreville na Zambia kutwaa taji hilo. 
Coulibaly kwasasa ana umri wa miaka 42, atakuwa anaweka rekodi ya mwamuzi aliyechezesha michezo mingi ya fainali za AFCON endapo atakabidhiwa tena filimbi nchini Afrika Kusini na bila shaka atafanya hivyo kwa kuwa ameshatajwa kwenye orodha.
Haya yatakuwa ni mashindano ya 7 kwake tangu aanze kuchezesha fainali hizi alipoitwa kwa mara ya kwanza mwaka 2002. 
Waamuzi wengine wapya walioitwa safari hii ni kutoka nchi jirani ya Kenya huyu ni Sylvester Kirwa na mwingine ni kutoka Seychelles Bernard Camille. 
Hivi ni kweli Kirwa ambaye alichezesha mchezo wa Star na Zambia mwezi Disemba mwaka jana ana kiwango kikubwa sana cha kumzidi Oden Mbaga wa Tanzania kama si kujidharau wenyewe na kutokuwa na tabia ya kujifanyia promo wenyewe.
Hii ndio faida ya kufagilia vya wenzetu sasa inatuponza.

Mwamuzi Oden Mbaga katikati.
Mwamuzi Izrael Mujuni mwenye mpira.
Algeria na Senegal zenyewe zina idadi kubwa ya waamuzi 3 kutoka kila nchi.
Algeria ina mwamuzi mzoefu Mohamed Benouza mbaye kwake hizi zitakuwa ni fainali za 5 kuchezesha wakati ambapo Diatta amekuwepo katika kila fainali tangu mwaka 2006. 
Zitakuwa ni fainali za tatu mfululizo kwa Bennett na za pili kwa Siwela. Wote pia wapo katika orodha fupi ya waamuzi walioteuliwa tayari kwa ajili ya fainali za kombe la dunia nchini Brazil mwaka 2014.
Sasa Sunday Kayuni narudi tena kwako ina maana zile semina za waamuzi ambazo wanakuja wakufunzi wa CAF na FIFA karibu kila mwaka hazina faida kwa watanzania? Na kama semina zinaandaliwa na CAF na FIFA tunashindwa kuwaambia ukweli au watuambiye kufanye namna gani ili kuhakikisha na sisi waamuzi wetu wanakuwepo michuano mikubwa na kuingia moja kwa moja katika mchakato wa kutangaza orodha ya waamuzi wa michuano kama hii.
Tanzania kupitia TFF ni wanachama wa CAF na FIFA na wewe ndio mkurugenzi wa ufundi kitengo ambacho ndiyo jiko na jicho la mpira wa nchi yoyote duniani pigania waamuzi wa nchi yako baba, waafrika tuna tabia ya uchoyo wenzetu wanatunyima kwa uchoyo wao tu lione hili. Si kweli kwamba hatuwezi, tunaweza sana isipokuwa tuko nyuma sana na tumekubali kunyimwa.
Au tumefutwa uanachama wa CAF na FIFA. Tunajiweka mbali sana na tunadhani mpira uko katika nchi fulani, huu ni utumwa wa mawazo. Ndio maana niliwahi kuandika katika moja ya makala yangu kuwa, TFF na shirikisho la baraza la vyaka vya soka Afrika mashariki na kati sasa umefika wakati wa kuacha kumuogopa Rais wa CAF Issa Ayatou hana faida kwenu na wala hakuna sababu ya kumuunga mkono mtu ambaye hajali soka la ukanda wenu.
Nilikuwa na maana ya kwamba mpira wa ukanda huu utaendelea kudumaa kwa kumuunga mkono Ayatou ambaye nyie kama viongozi mmeutangazia umma kuwa mtakwenda kumpa kura kwenye uchaguzi wa mwezi machi. Hiyo kura si ya watu wa Afrika mashariki na kati hizo kura ni zenu wenyewe. Hatumuungi mkono huyo mtu sisi.
Narudi kwenye mada kaka yangu Sunday Kayuni badilisha waamuzi wa Tanzania na pigania nafasi zao barani Afrika ni heshima kubwa kwao kuchezesha AFCON na si CECAFA na michezo ya vilabu Afrika.

No comments:

Post a Comment