Serikali imekubali mchakato wa
uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) uendelee kwa sharti la
kuhakikisha haki inatendeka kwa wagombea waliofika mbele ya Kamati ya Rufani ya
Uchaguzi.
Akizungumza na Waandishi wa Habari
leo mchana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema uamuzi huo umefikiwa kwenye
kikao kati ya uongozi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo chini
ya Waziri Dk. Fenella Mukangara, TFF na Baraza la Michezo la Taifa (BMT).
Amesema baada ya maafikiano hayo,
TFF italiandikia barua Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) ambalo
ndilo lililosimamisha mchakato huo ili litume ujumbe wake kwa ajili ya
kusikiliza malalamiko ya wagombea walioenguliwa.
Rais Tenga ambaye ameishukuru
Serikali kwa kuruhusu mchakato huo uendelee, pia ameahidi kuwa uchaguzi wa TFF
utafanyika kabla ya Mei 25 mwaka huu kama walivyokubaliana na Serikali, na kuwa
haki si tu itatendeka bali ionekane imetendeka.
“Serikali imetuelekeza uchaguzi
ufanyike kabla ya Mei 25. Tumewaambia kwetu huko ni mbali. FIFA wakija hata
kesho wakituambia endeleeni sisi tuko tayari. Hesabu zetu ziko tayari,
makabrasha yote yako tayari yanasubiri mkutano tu. Labda itakuwa kutoa muda tu
kwa wajumbe walioko mbali waweze kujiandaa, maana wajumbe huwezi kuwaita
ghafla,” amesema.
Amesisitiza kuwa TFF ilishapanga
tarehe ya uchaguzi, lakini ukasimamishwa na FIFA baada ya baadhi ya
walioenguliwa kulalamika huko. Hivyo maneno kuwa TFF hawataki uchaguzi kwa
sababu wanataka kuendelea kubaki madarakani haya maana hata kidogo.
Hivyo amewataka wagombea wote
waliofika kwenye Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na wakaendelea kujiandaa vizuri,
kwani FIFA watakapofika watawasikiliza wao na vyombo vilivyowaengua.
Pia amesema TFF ina heshimu Serikali
na itaendelea kufanya hivyo, lakini vilevile lazima iheshimu FIFA sababu iko
kwenye mpira wa miguu, na FIFA ndiyo wasimamizi wa mchezo huo duniani.
Amewakumbusha wanachama wa TFF, hasa
wajumbe wa Mkutano Mkuu kufahamu kuwa TFF ina katiba, lakini ni lazima pia
wafahamu kwanini kuna FIFA.
Rais Tenga amewahadharisha watu
wanaopitapita mikoani kuomba saini za wajumbe ili kuita Mkutano Mkuu wa dharura
wakati wanajua mkutano ulishaitishwa, lakini ukasimamishwa na FIFA. Jambo hilo
kikatiba ni kosa.
No comments:
Post a Comment