Shirikisho
la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) limefanya mabadiliko ya mwamuzi wa mechi
ya mchujo kusaka tiketi ya Fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ligi ya
Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes)
itakayochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mwamuzi
aliyeondolewa kutokana na sababu za kiufundi ni Jean Claude Birumushahu
aliyekuwa mwamuzi msaidizi namba moja. Nafasi yake sasa inachukuliwa na
Herve Kakunze pia kutoka Burundi.
CAF
imemuondoa mwamuzi huyo baada ya kufeli katika mtihani wa waamuzi
(Cooper Test) kwa waamuzi wa Burundi wanaotambuliwa na Shirikisho la
Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA) uliofanyika nchini humo siku tatu
zilizopita.
Waamuzi
hao na Kamishna wa mechi hiyo Gebreyesus Tesfaye kutoka Eritrea
wanatarajiwa kuwasili nchini kesho (Julai 11 mwaka huu) kwa ndege za
Kenya Airways na EgyptAir kwa muda tofauti.
Nayo
Uganda Cranes inatarajiwa kuwasili nchini kesho (Julai 11 mwaka huu) na
itafikia hoteli ya Sapphire. Shirikisho la Mpira wa Miguu Uganda (FUFA)
bado halijatuma taarifa rasmi juu ya ujio wa timu hiyo.
Wakati
huo huo, makocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen na wa Uganda, Milutin
Micho pamoja na manahodha wao watakuwa na mkutano na Waandishi wa Habari
utakaofanyika keshokutwa (Julai 12 mwaka huu) saa 5 asubuhi kwenye
ofisi za TFF kuzungumzia mechi ya Jumamosi.
No comments:
Post a Comment