Rais wa shirika linaloongoza mchezo wa mbio za magari duniani
FIA Jean Todt, atakabiliwa na upinzani mkubwa wa kutetea nafasi yake ya Urais mwezi Desemba, baada ya
David Ward kutangaza kugombea nafasi hiyo.
David Ward ambaye ni mkurugenzi mkuu wa shirika huru la hisani la
Taasisi ya FIA, amejiuzulu nafasi yake hiyo baada ya miaka 12, ili
apambane dhidi ya Todt. Ward mwenye umri wa miaka 56, alisema kipindi
cha uchaguzi kinaanza mwezi huu wa Septemba, na kwa hivyo ilikuwa muhimu
kwake kuwafikia wanachama wa FIA ili aweze kupata uteuzi.
Todt alimrithi Max Mosley kama rais wa FIA mwaka 2009, baada ya
kumshinda Ari Vatanen katika uchaguzi wa baraza kuu ya FIA, lakini
Mfaransa huyo bado hajathibitisha iwapo anataka kugombea muhula wa pili
baada ya muhula wake wa sasa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu. Ward
anajivunia mtandao mkubwa wa kisiasa ndani ya FIA, unaotokana na nafasi
yake ya zamani kama msaidizi wa Mosley.
Lotus yambembeleza Kimi Raikonnen
Na timu ya mashindano ya Lotus inafanya kila jitihada kumshawishi dereva
Kimi Raikonnen abaki katika timu hiyo msimu ujao, mkuu wa timu hiyo
yenye makao yake nchini Uingereza Eric Boullier amesema. Kumekuwa na
minon'gono ya hapa na pale kuhusu mustakabali wa dereva huyo, raia wa
Finnland mwenye umri wa miaka 33.
Wakati akisema anatumaini kuwa bingwa huyo wa dunia wa mwaka 2007
ataendelea kuwepo katika timu ya Lotus, Boullier alikri kuwa yapo
masuala kadhaa yasiyopatiwa ufumbuzi, ambayo yanapaswa kushughulikiwa
kabla ya kusaini mkataba mpya. Raikonnen yuko pointi 63 nyuma ya dereva
anaeongoza katika ubingwa, Sebastian Vettel kutoka Ujerumani.
No comments:
Post a Comment