Kiungo wa timu ya taifa ya soka ya Ujerumani, Mesut Ozil, amewashukuru
mashabiki wa klabu yake ya zamani, Real Madrid, na pia kuukosoa uongozi
wa klabu hiyo kufuatia uhamisho wake kwa timu ya Arsenal jijini London.
"Asanteni sana kwa miaka mitatu murwaa kabisa na nyinyi nyote. Wakati
wangu ulikuwa wa kipekee na maalumu sana kwangu. Wakati mwingine mambo
yanakwenda tofauti na vile nilivyotarajia siku chache zilIzopita,"
amesema Ozil katika taarifa yake aliyoitoa Jumatatu usiku (02.09.2013)
baada ya uhamisho huo.
"Nawatakieni nyote pamoja na timu kila la kheri. Sasa nina matarajio
makubwa na klabu yangu mpya: Wabeba Mizinga - Arsenal!" Mchezaji huyo wa
miaka 24 pia aliweka bayana siku ya Jumanne kwenye mahojiano na
televisheni ya shirikisho la soka la Ujerumani, dfb-tv, kuwa wakati
unafaa kuondoka Madrid kwa kuwa haonekani akifaa katika mipango ya kocha
mpya wa Real Madrid, Carlo Ancelotti. "Niligundua katika siku za hivi
karibuni sikuwa na uaminifu wa kocha. Arsenal wana imani hiyo na mimi
kwa hiyo nitakwenda kujiendeleza zaidi," amesema Ozil.
Ozil ni mchezaji wa Ujerumani anayelipwa kitita kikubwa
Arsenal ililipa rekodi ya paundi milioni 42.5, sawa na dola milioni 66,
kwa kiungo huyo wa timu ya taifa ya Ujerumani, ambaye amesaini mkataba
wa miaka mitano. Ozil anajiunga na wachezaji wenzake wa timu ya taifa ya
Ujerumani, Per Mertesacker na Lukas Podolski katika klabu ya Arsenal na
atavaa jezi nambari 11 mgongoni. Kiwango hicho ni kikubwa kuwahi
kulipwa kwa ajili ya mchezaji wa soka wa Ujerumani, kupita kile cha euro
milioni 37 ambacho mabingwa watetezi wa ligi ya Ujerumani, Bayern
Munich, waliilipa Borussia Dortmund kumpata Mario Goetze mapema mwaka
huu.
Ozil pia amekuwa mchezaji aliyeuzwa kwa gharama kubwa na Real Madrid.
Rekodi iliyokuwepo ilikuwa ikishikiliwa na mshambuliaji kutoka Brazil,
Robinho, ambaye alihamia Manchester City mwaka 2008 kwa kitita cha euro
milioni 43. Kuondoka kwa Ozil kulikamilishwa baada ya kuthibitishwa
uhamisho wa Gareth Bale hadi Real Madrid kutoka kwa mahasimu wa Arsenal
wa kaskazini mwa jiji la London, Tottenham Hotspur. Uhamisho huo uliweka
rekodi mpya ya euro milioni 100.
Hatua ya Ozil kuhamia Arsenal haingeweza kuepukika baada ya Real Madrid
kukataa kutilia maanani ombi la mchezaji huyo kutaka aongezwe mshahara.
Mashabiki wengi wa Real Madrid wametamaushwa na uhamisho wa Ozil huku
asilimia 66 walioulizwa kwenye utafiti wa maoni katika mtandao wa
intaneti uliofanywa na gazeti la michezo la As wakipinga uhamisho huo.
No comments:
Post a Comment