SIMBA KUMTAMBULISHA RASMI KIUNGO WAO WA ZAMANI HENRY JOSEPH SHINDIKA LEO.
Na. Ezekiel Kamwaga
Ofisa Habari
Simba SC
Mara baada ya safari
ya mikoa ya Tabora na Arusha kwenye mechi mbili za awali za Ligi Kuu ya
Tanzania, timu ya Simba imerejea salama jijini Dar es Salaam ikiwa na
kikosi chake kamili tayari kujiandaa na mechi ijayo ya ligi dhidi ya
Mtibwa Sugar ya Morogoro iliyopangwa kuchezwa Septemba 14 mwaka huu.
Kama sehemu ya maandalizi ya mechi hiyo, kikosi cha Simba kitashuka
dimbani katika Uwanja Mkuu wa Taifa siku ya leo, Jumatatu Septemba 2,
kucheza na Mafunzo ya Zanzibar katika mechi ambayo ina faida nyingine
zaidi ya kuwa ya kujiandaa na mechi ya Mtibwa.
Mchezo huo utatoa nafasi kwa wapenzi na wanachama wa Simba, pamoja na washabiki wa
soka kwa ujumla wake, kupata fursa ya kuwaona kwa mara ya kwanza
wachezaji wapya watatu wa klabu ambao hawajawahi kuonekana wakicheza
jijini Dar es Salaam.
Wachezaji hao ni Henry Joseph Shindika
aliyetoka Kongsvinger ya Norway, Gilbert Kaze na Amissi Tambwe waliotoka
katika klabu ya Vital’o ya Burundi. Ingawa hawa ni wachezaji wa Simba
lakini hawakutambulishwa katika Tamasha la Simba Day kama ilivyo ada kwa
wachezaji wote wapya.
Mechi ya Mafunzo itatoa fursa hiyo ya kutambulishwa na kuonekana wakiitumikia klabu kwa mara ya kwanza jijini hapa.
Pili, mechi hiyo itatumika na klabu kwa ajili ya mchezaji wake, Kiggi
Makassi, ambaye atawaaga washabiki rasmi kwa ajili ya safari yake ya
kwenda nchini India anakokwenda kwa matibabu ya goti lake. Kiggi
anatarajiwa kuondoka jijini Septemba tisa mwaka huu.
Kwa vile
Septemba 2 inaangukia siku ya kazi, waandaaji wa pambano hilo wamepanga
ianze saa 11 jioni ili kutoa nafasi kwa wapenzi wengi zaidi kuhudhuria
pambano hilo.
VIINGILIO
KATIKA pambano hilo viingilio vitakuwa
ni Sh 20,000 kwa VIP A, Sh 10,000 kwa VIP B, Sh 8,000 kwa VIP C na Sh
5,000 kwa mzunguko.
Maandalizi yote kwa ajili ya mechi yamekamilika na timu zote tayari ziko jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment