Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Kikosi
cha Taifa Stars kimewasili salama hapa Banjul, Gambia tayari kwa mechi
ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya wenyeji itakayochezwa kesho
(Septemba 7 mwaka huu).
Stars
inayodhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager imewasili hapa jana
(Septemba 5 mwaka huu) saa 11 jioni ikitokea Dakar, Senegal ambapo
ilichelewa kuunganisha ndege, hivyo kuamua kutumia usafiri wa barabara
kwa vile ni karibu na baadaye kupanda kivuko kuingia Banjul badala ya
kulala na kuchukua ndege nyingine siku inayofuata.
Wachezaji
wako katika hali nzuri na leo jioni wanatarajia kufanya mazoezi ya
mwisho kwenye Uwanja wa Independence ulioko Bakau ambao utatumika kwa
mechi ya kesho. Timu imefikia hoteli ya Seaview iliyoko kandokando ya
Bahari ya Atlantic.
Mechi
hiyo itaanza saa 10.30 jioni kwa saa za hapa ambapo nyumbani Tanzania
itakuwa saa 1.30 usiku, na itachezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda
Munyemana Hudu. Waamuzi wasaidizi ni Theogene Ndagijimana, Honore Simba
na Issa Kagabo. Kamishna ni Andy Quamie kutoka Liberia.
Washabiki
na vyombo vya habari vya hapa wanaizungumzia mechi hiyo ambayo ina
umuhimu mkubwa kwa pande zote, huku Gambia ikiwa imeita wachezaji tisa
wanaocheza barani Ulaya na Marekani. Gambia ambayo imepata uongozi mpya
wa Chama cha Mpira wa Miguu Gambia (GFA) imepania kuhakikisha haimalizi
mechi za mchujo ikiwa na pointi moja tu.
Kwa
upande wa Tanzania, Kocha Kim Poulsen amesema nia ni kuona Stars yenye
pointi sita inamaliza katika nafasi ya pili nyuma ya Ivory Coast ambayo
tayari imechukua tiketi pekee ya kucheza raundi ya mwisho kutoka kundi
hili la C.
“Mechi
hii ni muhimu kwetu kwa vile tunataka matokeo mazuri ugenini. Lakini
kikubwa ni kuwa matokeo mazuri si tu yatatuweka katika nafasi ya kuwa wa
pili, lakini vilevile yatatusaidia kuongeza pointi kwenye viwango vya
ubora vya FIFA, na kikubwa zaidi hii ni sehemu ya maandalizi ya sisi
kucheza Fainali za Afrika za 2015,” amesema Kim.
Stars
inatarajiwa kupangwa hivi; Juma Kaseja, Vincent Barnabas, Erasto Nyoni,
Nadir Haroub, Henry Joseph, Frank Domayo, Haruni Chanongo, Amri Kiemba,
Mrisho Ngasa, Simon Msuva na Khamis Mcha.
No comments:
Post a Comment