MSUGUANO wa mbio za Urais katika
Shirikisho la Soka nchini (TFF), umeendelea leo baada ya mgombea wa
nafasi hiyo kubwa katika ngazi ya mpira wa miguu Tanzania, Athman
Nyamlani kutaja vipaumbele tisa vya maendeleo ya soka, iwapo atapata
ridhaa ya wapiga kura
Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, katika Ukumbi wa Idara ya
Habari (MAELEZO), ikiwa sehemu ya uzinduzi wa kampeni zake za uchaguzi
utakaofanyika Jumapili, Nyamlani alisema akipewa nafasi hiyo, atainua
kiwango cha soka kwa kutekeleza msingi imara wa soka la Tanzania.
Nyamlani ambaye kitaaluma pia ni hakimu wa Mahakama ya Wilaya
Kinondoni, alisema katika kipindi cha miaka minne ataimarisha usimamizi
na Manejimenti ya soka katika ngazi zote kwa kupitia nafasi hiyo ya
urais sanjari na kushirikiana na viongozi wa klabu na vyama vya soka vya
wilaya na mikoa kwa ujumla wake.
Alisema ataimarisha usimamiaji na menejimenti ya soka katika ngazi
zote kwa kutoa mafunzo ya mara kwa mara kwa viongozi na kusimamia sheria
na taratibu za uendeshaji wa soka la Tanzania na suala la viongozi
kujiendeleza kielimu litapewa kipaumbele na litakuwa ni agenda endelevu.
Nyamlani alisema suala lingine ambalo litakuwa katika utekeleza wake ni rushwa katika soka nchini.
Nyamlani alisema suala lingine ambalo litakuwa katika utekeleza wake ni rushwa katika soka nchini.
“Naomba nikiri kuwa kumekuwa na malalamiko na vitendo vya rushwa
ambavyo vinawahusisha viongozi wa soka. Hivyo basi kwa kushirikiana na
serikali na viongozi wa soka katika ngazi zote nitahakikisha naendeleza
mapambano dhidi ya rushwa,” alisema Nyamlani.
Kipaumbele cha tatu kitakuwa ni kukuza soka la watoto, vijana na
wanawake, akiwa kama Rais wa TFF, atalipa uzito wa kipekee soka la
watoto wenye umri wa miaka chini ya 16 na soka la vijana na kukuza
vipaji kuanzia miaka tisa hadi 12, 13-14, 15-17 na 18-21 na soka ya
wanawake.
Nyamlani alisema kazi hiyo ataitekeleza kwa kuanzisha program mbali
za mashindano na za kukuza vipaji kwa makundi haya ya vijana kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali wa soka.
Kwa sababu kubwa ya kufanya hivyo ni ukweli kwamba haya makundi
ambayo yameonesha uwezo yatatoa mwanga jambo ambalo uongozi uliopita
ulilifanya na alihaahidi kuendeleza kulitekeleza kwa kushirikiana na
viongozi wa soka katika nagzi mbalimbali na serikali.
Kipumbele kingine muhimu ni Kuimarisha Uwezo wa Rasilimali Fedha wa
Shirikisho, kama Rais wa TFF atahakikisha kuwa TFF inapata vyanzo
endelevu na vya kuaminika ili kuweza kujenga uwezo wa shirikisho katika
kutekeleza mipango kikamilifu.
Nyamlani alisema ataimarisha idara ya masoko ili kuweza kupata wadhamini zaidi na kuweza kuuza nembo za shirikisho.
Alisema kipaumbele kingine ni Kuongeza Idadi na Ubora Waamuzi, Walimu wa soka na Wataalamu wa Afya ya Michezo.
Nyamlani alisema atahakikisha kunakuwa na program endelevu ya mafunzo
kwa makocha, waamuzi wa soka nchini na wataalamu wa afya ya michezo ili
kuongeza ufanisi wao katika kutekeleza majukumu yao kwa mujibu wa
sheria na taratibu zinazoongoza michezo wa soka, pia kufikia viwango vya
kimataifa vilivywekwa na Caf na Fifa.
Kipaumbele cha sita ni Kuongeza Ubora wa Ligi Kuu, Ligi Daraja la
Kwanza, Ligi za wilaya na mikoa, mashindano ya Ligi daraja la 1, ligi za
wilaya, mikoa na Ligi Kuu ni ngazi muhimu ya kukuza soka katika nchi.
Nyamlani alisema atashirikiana na viongozi wa soka na vyama vya
kitaalamu ili kuweza kuboresha kanuni mbalimbali zitakazowawezesha
wachezaji vijana kuwa wachezaji wa kulipwa.
Alitaja kipaumbele kingine ni Kuongeza Idadi ya Mawakala wa Wachezaji
ambao ni Watanzania, kama Rais wa TFF ana imani kwamba ili soka la
Tanzania likue kwa kasi ni lazima ataongeza idadi ya wachezaji na
mawakala wanaozingatia weledi.
Alisema ataimarisha Ushirikiano wa TFF na Serikali, kama rais wa TFF
atahakikisha anakuza na kuendeleza mahusiano mazuri kati ya TFF na
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa imani kwamba ni jambo
hilo ni muhimu kwa ustawi wa soka kwa sababu ni ukweli soka sasa ni
ajira kwa vijana ambao ni nguzo ya Taifa.
Kipaumbele cha tisa ni Kuimarisha Ushirikiano wa TFF, Caf na Fifa,
atahakikisha kuwa anakuza na kuendeleza mahusiano kati ya vyombo hivyo
ili kuongeza kasi ya ukuaji wa soka nchini, kufikia viwango vya
kimataifa kwa kutumia misaada mbalimbali ya kitaalamu na kifedha
inayotolewa na Taasisi hizo kubwa duniani.
No comments:
Post a Comment