Mahakama ya Rufaa nchini Tanzania imetupilia mbali
ombi la warufani wawili Nguza Viking na mwanaye, ambao waliomba mahakama
hiyo kufanya marejeo ya uamuzi wake wa awali wa kuwapata na hatia kama
ambavyo hukumu dhidi yao ilivyotolewa na mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu
mwaka 2004.
Nguza Viking, maarufu kama Babu Seya na watoto
wake watatu walihukumiwa kifungo cha maisha jela kwa makosa ya kubaka na
kulawiti watoto.
Mwaka 2010, rufaa yao ilisikilizwa
katika Mahakama ya Rufaa, na kuwaachia huru Nguza Mashine na Francis
Nguza baada ya kuwaona hawana hatia katika makosa yote waliyoshitakiwa.
Baada ya rufaa hiyo, Babu Seya na mwanaye Papii
Kocha walipatikana na hatia na hivyo kuendelea kutumikia adhabu ya
kifungo cha maisha jela.
Tarehe 30 Oktoba mwaka huu, Mahakama ya Rufaa
iliyoketi chini ya jopo la majaji watu, likiongozwa na Nathalia Kimaro,
akisaidiana na Mbarouk Mbarouk na Salum Masati walisikiliza hoja za
pande zote kuhusu ombi la kufanyika mapitio ya uamuzi wa awali wa
mahakama hiyo.
Alhamisi, Mahakama ya Rufaa baada ya kufanya
mapitio ikiwa imeketi chini ya majaji watatu, imeendelea kuwaona
warufani hao wawili kuwa na hatia na hivyo kuendelea kutumikia adhabu
yao.
Upande wa utetezi ukiongozwa na wakili wao
Mabere Marando uliomba kupitiwa upya kwa uamuzi huo, ukidai kuwepo
kasoro katika ushahidi uliowatia hatiani, ikiwemo kukosekana kwa
mashahidi muhimu katika kesi hiyo.
Majaji walisema kuwa kuna uthibitisho kuwa warufani hao wawili waliwabaka watoto wa shule ya msingi mwaka 2003.
Kesi hiyo imewashtua mashabiki wa mwanamuziki Viking nchini Tanzania na kanda nzima ya Afrika Mashariki.
Mwanamuziki huyo mwenye kuimba nyimbo za Rhumba,
ambaye ni mzaliwa wa DRC, ameishi Tanzania kwa miaka mingi na kuwa na
mashabiki wengi.
Mwandishi wa BBC Ben Mwang'onda mjini Dar es
Salaam anasema kuwa Nguza Viking na mtoto wake Johnson Nguza maarufu
kama Papii Kocha ambaye pia ni mwanamuziki, walifika mahakamani hapo
kusikiliza hatma yao.
Walionekana kuwa watulivu wakati majaji walipotupilia mbali ombi lao kutaka hukumu yao kubatilishwa.
Walihukumiwa kwa kuwabaka wasichana 10 wa shule
ya msingi waliokuwa kati ya umri wa miaka sita na nane wote waliokuwa
katika shule ya msingi ya Mashujaa wilayani Kinondoni mjini Dar es
Salaam.
Wakili wa muimbaji huyo alisema kuwa mwanamuziki huyo hana matumaini tena ya kupewa rufaa kwani hili ndilo ombi lake la mwisho.
No comments:
Post a Comment