Timu ya taifa ya Tanzania Bara The Kilimanjaro Stars hii leo imelazimishwa kwenda sare na timu ya taifa ya Zambia maarufu kama Chipolopolo katika mchezo wao wa kwanza wa michuano ya Chalenji inayoendelea nchini Kenya huku kila upande ukiambulia alama moja.
Huo ulikuwa ni mchezo wa kundi B wa michuano hiyo uliopigwa katika uwanja wa Machakos, huku Chipolopolo wakiwa ndio wa kwanza kuandika bao dakika nne mara baada ya kuanza kwa mchezo huo ambapo bao la Chipolopolo likifungwa na Ronald Kampamba kwa kichwa kufuatia kupokea krosi ya Felix Katongo kutoka upande wa kushoto.
Kilimanjaro walisawazisha bao hilo katika dakika ya 15 ya kipindi cha pili kwa kichwa na Saidi Moradi baada ya kupokea mpira wa kona.
Pande zote mbili walijaribu kuitawala mchezo lakini walishindwa kufanya hivyo kutokana na pichi ya uwanja wa Machakos kutifuka kutoka na mvua zinazoendelea kunyesha nchini Kenya.
Katika mchezo wa kwanza Burundu Intamba Murugamba walifanikiwa kuwachapa Somalia kwa mabao 2-0 na hivyo kwa matokeo hayo sasa Burundi watakuwa wakiongoza kundi hilo.
Hayo si matokeo mazuri kwa Zambia ambao ni mabingwa wa Afrika wa mwaka 2012 hii ni kutokana na ukweli kwamba huu ni mchezo wao wa tisa wakishindwa kupata ushindi.
Kikosi cha Patrice Beaumalle kilishinda 2-0 mwezi Agosti dhidi ya Botswana 2-0 mchezo wa kuwania kufuzu fainali za Chan 2014 mjini Ndola.
Tangu wakati huo walikwenda sare mbili kabla ya kupoteza michezo mitano dhidi ya Zimbabwe, Ghana, Brazil, Jordan na Misri.
Zambia wataumana na Burundi katika mchezo wao unaofuata wa kundi B Desemba mosi kabla ya kumaliza dhidi ya Somalia siku nne baadaye.
No comments:
Post a Comment