David Moyes amekanusha kwamba uhusiano wake na nyota wa kikosi chake
umezorota akisema kuwa wachezaji wake wanamuunga mkono, huku shinikizo dhidi ya meneja
huyo wa magwiji, Manchester United, likiendelea.
Moyes amekumbwa na mashaka tangu kuchukua kazi ya kukiongoza kikosi cha mabingwa hao
wa Ligi ya Premier ya Uingereza Julai na mwaka mpya umemwongezea
majonzi.
United wamepoteza mechi tatu mtawalia za kufungua mwaka kwa mara ya
kwanza tangu 1932 huku Tottenham, Swansea katika kombe la FA na
Sunderland katika lile la League Cup wakiwatepetesha kabisa.
Licha ya hayo, Moyes ameshikilia kwa dhati kwamba hajapoteza utawala
wa wachezaji wake ambao hawana uzoefu wa kuchakazwa kila kuchao.
“Sidhani wachezaji wamejificha,” meneja huyo ambaye klabu chake kina
mwanya wa pointi 11 nyuma ya viongozi wa Premier, Arsenal, alisema.
“Kila mmoja wao amesimama kidete na kufanya kila liwezekanalo.
Hauwezi kuamrisha yeyote atie bidii zaidi ya uwezo wake na vijana wangu
wamekuwa wakifanya hivyo,” aliongeza.
Huku Arsenal wakisubiri hadi Jumatatu kucheza kwenye ligi watakapo
watembelea Aston Villa, Chelsea, wanaoketi nafasi ya tatu wana nafasi ya
kumiliki uongozi ikiwa watatamba ugenini Hull City Jumamosi.
No comments:
Post a Comment