Rais wa Shirikisho la Soka duniani FIFA Sepp Blatter, amedokeza
kwamba anapanga kugombea tena kama rais wa shirikisho hilo kwa muhula wa tano akidai kuwa
bado hajakamilisha majukumu yake
Blatter amenukuliwa na gazeti moja nchini Uswisi akisema kuwa angependa
kugombea, kwa sababu kazi bado haijakamilika. Blatter mwenye umri wa
miaka 78 amesema mamlaka yake yanafikia ukingoni, lakini jukumu lake
halijakamilika.
Mswisi huyo amekuwa katika uongozi wa FIFA tangu mwaka wa 1998.
Uamuzi
wake wa kuashiria kuwa atagombea, unakuja zikiwa zimesalia wiki chache
tu kabla ya kuanza kwa fainali za Kombe la Dunia nchini Brazil Juni 12.
Uchaguzi huo utaandaliwa mwaka wa 2015.
Mgombea pekee ambaye amejitosa rasmi katika kinyang'anyiro
hicho ni Jerome Champagne, katibu mkuu wa zamani wa FIFA, aliyestaafu
mwaka wa 2010.
Macho hata hivyo yataangaziwa rais wa Shirikisho la Soka
Ulaya – UEFA Michel Platini ambaye alidai kuwa yeye ndio mtu pekee
anayeweza kumpiku Blatter katika uchaguzi.
Lakini Mfaransa huyo
hajafanya uamuzi kama atagombea akisisitiza kuwa atatoa msimamo wake
baada ya Kombe la Dunia.
Waakti huo huo Shirikisho la Soka Ulimwenguni FIFA linaamini kuwa Brazil
itakuwa tayari kuandaa dimba la Kombe la Dunia mwezi ujao wakati
ikiharakisha kumalizia kwa wakati unaofaa ujenzi wa viwanja vyote 12.
Katibu Mkuu wa FIFA Jerome Valcke amesema kila kitu hakijakamilika kwa
kinyang'anyiro hicho kinachong'oa nanga Juni 12 hadi Julai 13. Siku ya
Alhamis, Polisi nchini Brazil walifanya mgomo wa saa 24 wakidai
mazingira bora ya utendaji kazi, ikiwa ni siku 37 pekee kabla ya nchi
hiyo kuandaa dimba la Kombe la Dunia.
Polisi imetishia tena kugoma
wakati wa tamasha hilo la soka la kimataifa. Polisi waligoma katika miji
kadhaa itakayoandaa Kombe la Dunia pamoja na mji mkuu Rio, ambao
utaandaa mechi saba ikiwemo fainali ya dimba hilo mnamo Julai 13.
No comments:
Post a Comment