Arjen Robben amekiri kuwa alidanganya timu yake ikapewa penalti |
Huwa siyo jambo la kawaida kwamba mchezaji anaweza kujitokeza hadharani
na kuungama kwamba alipiga mbizi ili kutafuta penalti katika mchezo,
lakini hivyo ndivyo alivyofanya mshambuliaji wa Uholanzi Arjen Robben
Laana ya duru ya mchujo kwa vijana wa Mexico katika Kombe la Dunia bado
haijavunjwa kabisa. Huku wakicheza katika raundi ya pili kwa mara ya
sita mfululizo katika mchezo huo, Wamexico walionekana ni kama hatimaye
wamefanya sawa kila kitu walichohitaji kukifanya dhidi ya Uholanzi.
Ulinzi wao imara ulikuwa umeyazuia mashambulizi ya Waholanzi, huku
mlinda lango Guillermo Ochoa akiokoa makombora makali yaliyoelekzwa langoni mwake.
Wamexico
walipata goli kupitia kwa Giorvani Dos Santos katika kipindi cha kwanza
baada ya kufanya shambulizi baada ya jingine katika lango la vijana wa
Louis Van Gaal.
Mwamuzi aliusimamisha mchezo huo mara mbili
angalau wachezaji waweze kukata kiu kutokana na joto kali mjini
Fortaleza.
Dakika ya 88, Ochoa alishindwa kuzuia shuti kali la Wesley
Sneijder aliyefanya mambo kuwa 1-1. Dakika chache baadaye, Klaas
Jan Huntelaar aliwafungia Waholanzi bao la ushindi kupitia penalty
katika dakika za majeruhi, baada ya Arjen Robben kuangushwa na Rafael
Marquez. Kocha wa Mexico Miguel Herrera amelalamika sana kwamba penalty
hiyo ilikuwa ya kubuniwa tu.
Robben akizungumza baada ya mechi, alikiri
kuwa ni kweli alipiga mbizi mara kadhaa katika kipindi cha kwanza, na
jambo hilo limemsikitisha sana.
Ameomba radhi kuhusiana na tabia hiyo,
na lakini amesisitiza kuwa penalty yake iliyowapa ushindi ilikuwa
halali. Huyu hapa Robben
Uholanzi sasa watapambana Jumamosi mjini Salvadore na Costa Rica ambao
waliwashangaza wengi kwa kuwabandua nje Ugiriki katika mechi ambayo
iliamuliwa na mikwaju ya penalti.
Vijana hao wa Amerika ya kati
walicheza kwa kujituma licha ya kuwa walikuwa wamechoka sana kutokana na
kibarua walichokifanya cha kulinda lango lao baada ya kiungo Oscar
Duarte kutimuliwa uwanjani.
Mechi hiyo ilikamilika kwa sare ya goli moja kwa moja katika muda wa
kawaida na wa ziada. Costa Rica walifunga penalty zao zote tano, kabla
ya kuokolewa na shujaa wao mlinda lango Keylor Navas aliyezuia penalty
moja ya Ugiriki.
No comments:
Post a Comment