Rais wa shirikisho la soka duniani FIFA Joseph Sepp
Blatter, amesema anaamini mshambuliaji kutoka nchini Uruguay, Luis Alberto Suarez
Diaz atarejea katika kiwango chake cha kawaida licha ya kukabiliwa na adhabu
kali ya kufungiwa kwa miezi baada ya kubainika alimng’ata kwa makusudi beki wa timu ya taifa ya Italia
Giorgio Chiellini.
Blatter, amesema hayo kwa lengo la kupoza
machungu ya baadhi ya mashabiki wa soka duniani ambao wameonyesha kupingana na
adhabu iliyotolewa dhidi ya Luis Suarez, ambaye amefungiwa kwa muda wa miezi
minne kutojihusisha na masuala ya mchezo wa soka pamoja na kutokucheza michezo
tisa ya kimataifa.
Kiongozi huyo wa FIFA pia amepongeza kitendo cha
mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, cha kutambua makosa yake na kufikia
hatua ya kumuomba radhi Giorgio Chiellini.
Amesema Luis Suarez, ameonyesha uungwana mkubwa ambao
haukutarajiwa kutoka kwake, hivyo bado anaamini hatua hiyo ya kuomba msamaha
itamrejesha katika mustakabali mzuri wa kucheza soka lake mara atakapomaliza
adhabu inayomkabili.
Wakati huo huo shirikisho la soka duniani FIFA, limelegeza
adhabu ya mshambuliaji Luis Suarez, kwa kumruhusu kujumuika na wachezaji
wenzake wa klabu ya Liverpool kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kujiandaa kabla
ya kurejea tena uwanjani mwanzoni mwa mwezi novemba mwaka huu.
FIFA wamechukua maamuzi ya kumruhusu Suarez kufanya mazoezi
ya wachezaji wenzake wa Liverpool baada ya kuona upo umuhimu kwa mshambuliaji
huyo, kupewa haki kufanya mazoezi kutokana na mchezo wa soka kuchukua sehemu
kubwa ya maisha yake, hivyo kama atakuwa nje kwa muda wa miezi minne huenda
kiwango chake kikaporomoka.
Wakati huo huo imeelezwa kwamba uongozi wa FC Barcelona
umefikia makubaliano na viongozi wa klabu ya Liverpool, katika mazungumzo ya
kutaka kumsajili mshambuliaji Luis Suarez.
Taarifa zilizotangazwa na kituo cha radio cha Cadena Ser zimeripoti
kwamba viongozi wa FC Barcelona, wamekubali kutoa kiasi cha paund million 90
kama ada ya usajili wa mshambuliaji huyo ambae msimu uliopita aliibuka kinara
katika upachikaji wa mabao nchini Uingereza.
Taarifa za kituo hicho ziliambatana na uthibitisho wa
muwakilishi wa viongozi wa FC Barcelona, José Ramón de la Morena ambaye alikuwa
safarini kurejea nchini Hispania kitokea jijini London nchini Uingereza ambapo
kikao cha pande hizo mbili kilifanyika tangu mwanzoni mwa juma hili.
No comments:
Post a Comment