Mchezaji wa zamani wa klabu ya Gor Mahia na timu ya
taifa ya Kenya Haraambee Stars, Austin Oduor, amesema mshambuliaji
matata wa timu ya taifa ya Ubelgiji Divorc Origi ameiva kucheza katika
ligi kuu ya England.
Oduor, ambaye ni mjomba wake Origi, anasema
tofauti na maoni ya wengine kwamba mchezaji huyo angali mbichi kucheza
ligi kuu ya England kwake yeye anaona yuko tayari kabisa.
“Nimefuatilia mechi zote alizocheza
kufika sasa katika kombe la dunia na sina shaka kijana huyu wa ndugu
yangu(Mike Okoth) anaweza kucheza ligi kuu ya England bila tatizo kwa
sababu ana mwili mzuri, nguvu, akili ya mshambuliaji na kasi itakikanayo
kwa ligi kama hiyo,’’ asema Oduor.
''Asipoteze muda wake kwa sababu huu ndio umri
mzuri kwake kushiriki ligi hiyo. Nitazungumza naye na babake baada ya
kombe la dunia kwani singetaka tuanze kuzungumzia mengine wakati huu ila
kombe la dunia tu.’’
Baadhi wanahisi kuwa Origi bado ni mbichi ingawa ameonyesha kipawa chake Brazil
Origi, mwenye umri wa miaka 19 ameonyesha mchezo
mzuri kwenye mashindano ya kandanda ya kombe la dunia nchini Brazil, na
kwa mara ya kwanza alicheza dakika zote tisini dhidi ya Marekani kwenye
mechi yao ya raundi ya pili, na hatimaye Romelu Lukaku akaingia
uwanjani naye Origi akapumzika.
Miongoni mwa timu za ligi kuu ambazo zimeonyesha
nia ya kumsajili Origi ni Liverpool, Tottenham Hotspurs na Arsenal
lakini kuna dalili Liverpool itamnasa kinda huyo ambaye alizaliwa
Ubelgiji wakati babake Mike Okoth, raia wa Kenya, alipokuwa akicheza
kandanda ya kulipwa nchini humo.
Origi mwenyewe anasema ana hamu sana ya kushiriki ligi kuu ya England bora apate klabu kitakachomfurahisha.
Babake Origi ni shabiki sugu wa Liverpool hivyo
basi huenda akamshawishi mwanawe ajiunge na bingwa hao mara 18 wa ligi
kuu ya England.
Lakini kabla mashindano ya kombe la dunia yaanze
Okoth alisema atampa Origi uhuru wa kuamua ni klabu kipi anataka
kuchezea England endapo atakiacha kile cha Ufaransa, Lille.
No comments:
Post a Comment