TAARIFA KWA VYOMBO
UFAFANUZI KUHUSU MAAMUZI YA KAMATI YA UTENDAJI
Vyombo kadhaa vya habari vimeripoti kuhusu hali
ya mgongano kati ya Kamati ya Utendaji ya TFF na Bodi ya ligi Tanzania
(Tanzania Premier league Board).
Shirikisho la mpira wa miguu Tanzania linapenda
kutoa ufafanuzi ufuatao:
1.Bodi ya ligi imeundwa kwa mujibu wa Katiba ya
TFF kifungu 40(11).Hivyo Bodi ya ligi ni zao la Mkutano Mkuu wa TFF.
2.Katiba ya TFF imeipa mamlaka kamati ya utendaji ya TFF kutunga kanuni za
uendeshaji wa Bodi ya ligi,kanuni hizi ndiyo nguzo kuu ya uendeshaji wa
shughuli za Bodi ya ligi na ndizo zinaipa Bodi uhalali wake wa kuendesha
shughuli zake za kila siku.
3.Bodi ya ligi ni chombo cha TFF kama vilivyo
vyombo vingine vikiwemo kamati mbali mbali za TFF.Kisheria Bodi ya ligi sio
chombo huru (its not a legal entity) hivyo Bodi pamoja na mambo mengine haina
mamlaka ya kuingia mikataba ya aina yoyote ya kisheria .
4.Katiba ya TFF inatamka kuwa Bodi ya ligi
itaheshimu na kufuata maagizo ya TFF.Maagizo haya yanatolewa na Sekretarieti ya
TFF kwa niaba ya kamati ya utendaji ya
TFF.
5.Mwenye mamlaka ya kutengua maamuzi ya kamati ya
utendaji ya TFF ni Mkutano Mkuu wa TFF peke yake,hakuna chombo kingine cha
chini chenye mamlaka hayo.
6.Kanuni za mashindano zinaandaliwa na kamati ya
mashindano ya TFF na kupitishwa na kamati ya utendaji ya TFF. Kikao cha kamati
ya utendaji kilichopitisha rasimu ya kanuni za ligi za mwaka 2014/15
kilihudhuriwa na Mwenyekiti wa bodi ya
ligi,Makamu mwenyekiti wa Bodi ya
ligi na pia Mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya TFF,hawa wote ni wajumbe wa
Bodi ya ligi na walishiriki kikamilifu katika kikao cha kamati ya utendaji
kilichopitisha kanuni za ligi 2014/15 ukiwemo na utaratibu wa mgawanyo wa
mapato ya milangoni na ya udhamini.Katiba
ya TFF inaagiza hivyo kuwa Viongozi wakuu wa Bodi ya ligi watakuwa pia ni wajumbe wa kamati ya utendaji ya TFF.
Aidha mtendaji mkuu wa Bodi ya ligi alikuwepo kwenye kikao hiki cha kamati ya
utendaji kama mwajiriwa.
7. Uamuzi wa kuunda mfuko maalum wa kuendeleza
soka la vijana ni uamuzi uliopitishwa na kamati ya utendaji.Lengo la kuanzishwa
mfuko huu ni kuwa na chombo maalum ambacho kitakuwa kinakusanya fedha toka
vyanzo mbali mbali kwa ajili ya kuendeleza miradi ya soka la vijana nchini.Kwa
sasa miradi hii ni:
(a) Kuanzisha vituo vya kulea na kuendeleza
vipaji vya watoto kuanzia miaka 8-17
(sports centres) katika kila mkoa nchini mwetu.Mradi huu ni mkubwa
utahitaji nyenzo hasa walimu na vifaa.
(b) Kuandaa timu ya taifa umri chini ya miaka
12 kwa ajili ya mashindano ya Afrika
umri chini ya miaka 17 mwaka 2019. Timu hii itaanza kuandaliwa mwaka huu
Desemba baada ya mashindano ya kitaifa umri chini ya miaka 12. Hii timu
itakusanywa na kuwekwa katika shule moja ya bweni ambapo watalelewa na
kuendelezwa vipaji vyao wakiwa pamoja huku wanasoma.Tanzania tumeomba kuwa
wenyeji wa fainali hizi.
(c) Kuandaa timu ya Taifa umri chini ya miaka 14
kwa ajili ya michuano ya awali mwaka 2016 kuelekea fainali za Afrika umri chini
ya miaka 17 mwaka 2017.
(d) Kuandaa timu ya Taifa umri chini ya miaka 17
kwa ajili ya michuano ya awali mwaka 2016 kuelekea fainali za Afrika umri chini
ya miaka 20 mwaka 2017.
(e) Kuandaa mashindano ya Taifa ya mpira wa
wanawake na ligi ya taifa ya mpira wa wanawake.
Miradi yote hii muhimu kwa maendeleo ya mpira wa
miguu Tanzania haina udhamini lakini ni lazima ifanyike ili tujihakikishie
tunainua mpira nchini mwetu.Mafanikio ya miradi hii sio tu yatafaidisha na
kuimarisha timu zetu za Taifa lakini pia yatakuwa chimbuko madhubuti la wachezaji mahiri wa vilabu vyetu vya mpira
wa miguu.
Kimsingi tunatarajia kuwa vyanzo vikuu vya mapato
ya kutunisha mfuko wa maendeleo ya mpira Tanzania vitakuwa:
-
Mapato yatokanayo na mechi za ligi zetu madaraja
yote
-
Mapato yatokanayo na mechi za kimataifa
-
Wadhamini
-
Serikali kuu kupitia bajeti za Wizara zenye
dhamana ya michezo,halmashauri na vyuo
-
Wafadhili
-
Shughuli mbali mbali za kutunisha mfuko.
Kamati ya
utendaji ya TFF ilimteua Bwana Leodeger Tenga kuwa mwenyekiti wa kwanza wa
mfuko huu na wajumbe wake ni Bw Tarimba Abbas, Bw Ephraim Mafuru, Mzee Ayoub
Chamshama Bw Frederick Mwakalebela na Mh
Zarina Madabida. Bw Henry Tandau na Bw Boniface Wambura ni waratibu wa mfuko
huu. Imani ya TFF ni kuwa wajumbe hawa kwa kutumia uzoefu wao katika uongozi wa
jamii watatusaidia kuhakikisha mfuko huu unaanza vyema shughuli zake.
Upande wa
TFF tumefungua akaunti maalum benki kwa ajili ya kuingiza fedha zote
zinazokusanywa kama mchango wa TFF kwenye mfuko huu zikiwemo asilimia 5 za
makato ya fedha za udhamini na ZILE zitokanazo na mfuko wa jichangie,TFF inatoa
wito kwa wadau wote wa mpira wa miguu Tanzania kuchangia mfuko huu ili utumike
kunusuru mpira wetu. Fedha zitakazokusanywa matumizi yake yatasimamiwa na
kanuni za uendeshwaji wa mfuko huu.
Hitimisho:
Kila
mwanafamilia wa TFF anawajibika
kuheshimu na kufuata maelekezo ya Kanuni za mashindano ya ligi kuu kama
zilivyopitishwa na Kamati ya Utendaji ya TFF .Hivyo utaratibu wa mgawanyo wa mapato yatokanayo na
fedha za milangoni na za wadhamini kama ulivyoainishwa kwenye kanuni hizi uko
pale pale. Ninaiagiza Bodi ya ligi kusimamia utekelezaji wa maagizo ya Kamati
ya utendaji ya TFF mara moja. Mwenye malalamiko kuhusu kanuni hizi ayalete kwenye vyombo husika vya TFF kwa kufuata Katiba,kanuni na taratibu
za Shirikisho.Sote tunajenga nyumba moja hakuna haja ya kugombea fito.
Jamal
Malinzi
Rais wa TFF
Dar es
salaam
02/October/2014
No comments:
Post a Comment